Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili | Magazetini | DW | 14.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Afrika katika magazeti ya Ujerumani juma hili

Mapigano makali yazuka katika jimbo la Darfur nchini Sudan. Ugonjwa wa ebola wazuka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Askofu mkuu wa Bulawayo nchini Zimbabwe, Pius Ncube, ajiuzulu. Na tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya yapata pigo kubwa.

Naam tunaanza na kuzuka kwa mapigano huko Darfur. Gazeti la Neue Zürcher lilisema kuzuka kwa mapigano hayo kunahatarisha mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi ujao mjini Tripoli, Libya.

Siku moja baada ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuzungumzia ufanisi katika kuifikia amani katika jimbo la Darfur, mashambulio mapya ya mabomu yalifanywa na jeshi la serikali ya Sudan katika eneo la Hanskanita kulipiza kisasi mashambulio dhidi ya kambi ya jeshi hilo ya Wad Banda yaliyofanywa na waasi wa kundi la Haki na Usawa, Justice and Equality Movement, JEM, linaloongzwa na Khalil Ibrahim na kitengo cha kundi la Sudanese Libertaion Army, SLA.

Kwa mujibu wa kamanda wa kundi la JEM, Abdelaziz Ushar, ndege za kivita na helikopta zilitumiwa kufanya mashambulio ya angani huko Haskanita. Afisa wa Umoja wa Afrika katika anayefanya kazi Haskanita amethibitisha kufanywa mashambulio hayo ya mabomu dhidi ya mji huo.

Taarifa ya pili inahusu kuzuka kwa ugonjwa wa ebola katika jimbo la Kasai mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Gazeti la Frankfurter Rundschau lilisema shirika la afya duniani, WHO, lilisema watu 166 walifariki katika hali isiyoeleweka katika miezi minne iliyopita na wengine 400 wakaambukizwa homa kali pamoja na ugonjwa wa kuendesha na kutokwa na damu.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mjini Kinshasa ilisema matokeo ya uchunguzi uliofanywa na mahabara ya Atlanta nchini Marekani yalidhihirisha kwamba ugonjwa huo ni ebola. Karantini ilitangazwa katika eneo lililoathirika jimboni Kasai kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.

Gazeti la Tageszeitung lilizungumzia juu ya kuundwa miungano huku kukiwa na usitishwaji mapigano kati ya waasi wa jenerali Laurent Nkunda na majeshi ya serikali mashariki mwa nchi hiyo. Mhariri wa gazeti hilo alisema nchi jirani zinajipanga kuziunga mkono pande hizo zinazopigana mashariki mwa Kongo. Huku Uganda na Angola zikiwa upande wa serikali ya mjini Kinshasa, Rwanda kwa upande wake inawamuunga mkono waasi wanaoongozwa na jenerali Laurent Nkunda.

Taarifa ya tatu inahusu kujiuzulu kwa askofu mkuu wa Bulawayo nchini Zimbabw, Pius Ncube. Gazeti la Neue Zürcher lilisema Pius Ncube ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa rais Robert Mugabe, alijiuzulu kama askofu wa Bulawayo Jumanne iliyopita. Makao makuu ya kanisa Katoliki huko Vatican yamesema kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, Papa Benedict XVI amekubali kujiuzulu kwa askofu Ncube.

Askofu Ncube alichukua aumuzi huo baada ya gazeti la serikali ya Zimbabwe, The Herald, kuripoti kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mfanyakazi wake mwanamke. Katika taarifa yake askofu Ncube alisema ameamua kujiuzulu ili kulilinda kanisa Katoliki kutokana na aibu nyingine zinazoweza kutokea kufuatia kashfa yake.

Hata hivyo askofu huyo alisema hiyo ni kampeni iliyopangwa na serikali kumchafulia jina na kuliaibisha kanisa Katoliki. Amesisitiza kuwa kampeni hiyo haitamnyamazisha na ingawa amejiuzulu wadhifa wa askofu mkuu wa Bulawayo, anataka kuendelea kubakia askofu. Ili kuwasaidia wanachi askofu Pius Ncube anapanga kuunda shirika jipya la kutoa misaada.

Gazeti la Tageszeitung lilisema ingawa Pius Ncube amepoteza kazi yake kama askofu mkuu wa Bulawayo, baada ya kuhudumu kwa kipindi cha miaka kumi, askofu huyo ameapa hatanyamaa kimya katika kuikosoa serikali ya rais Mugabe.

Tunamalizia na hatua ya wabunge nchini Kenya kujilinda kwa kupitisha mswada wa sheria unaoizuia tume ya kupambana na rushwa nchini Kenya isichunguze kesi za rushwa kuanzia mwaka wa 2003. Gazeti la Neue Zürcher linasema baada ya kupitisha mswada utakaowawezesha kupata donge nono kama kifuta jasho kwa kuwa wabunge huku uchaguzi mkuu ukikaribia nchini humo, wabunge sasa wamejikinga kutokana na mkono wa sheria kwa kuizuia tume hiyo kuchunguza kesi za rushwa.
 • Tarehe 14.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHRp
 • Tarehe 14.09.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHRp