1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Merkel nchini Urusi yaingia utata

22 Juni 2013

Ziara ya Kansela Angela Merkel nchini Urusi hivi leo imeingia utata, baada ya kufutwa kwa hotuba ya uzinduzi wa sanamu la Enzi ya Shaba mjini Petersburg, kutokana na mgogoro wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

https://p.dw.com/p/18tv7
Bundeskanzlerin Angela Merkel (CDU) wird am 16.11.2012 im Kreml in Moskau von Russlands Staatspräsidenten Wladimir Putin bei den 14. deutsch-russischen Regierungskonsultationen begrüßt. Es ist Merkels erster Besuch in Moskau seit Putins erneutem Amtsantritt im Mai. Sie wird von acht Ministern und einer Wirtschaftsdelegation begleitet. Foto: Kay Nietfeld/dpa
Angela Merkel bei Wladimir Putin in Kreml Archiv 2012Picha: picture-alliance/dpa

Kansela Merkel na Rais Vladimir Putin wa Urusi walikuwa wahutubie jukwaa la wawekezaji mjini Saint Petersburg hivi leo, lakini sasa ziara ya Kansela huyo wa Ujerumani inaonekana kutatizika, baada ya kufuta uzinduzi wa maonyesho uliokuwa umeshapangwa awali.

Sasa Merkel hatafungua tena maonyesho yajuilikanayo kama Enzi za Shaba - Ulaya bila Mipaka kutokana na suintafahamu kati ya maafisa wa Ujerumani na wale wa Urusi juu ya nani anastahiki kutoa hotuba ya ufunguzi kati ya Merkel na Putin.

Hata hivyo, kwa mujibu wa msemaji wa Kansela Merkel, Steffan Siebert, sehemu nyengine ya ratiba ya Kansela Merkel inabakia kama kawaida. Merkel anatarajiwa kuhutubia kikao cha Jukwaa la Kimataifa la Kiuchumi la Saint Petersburg majira ya saa 9:00 kwa saa za Ulaya ya Kati.

Maonyesho hayo yaliyokuwa yafanyike kwenye jengo la Makumbusho la Ermitage mjini Saint Petersburg, yanajumuisha vitu vilivyoibiwa na wanajeshi wa Kisovieti wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Jumla ya vitu vya kikale 1,700 kutoka makumbusho mbalimbali duniani vinaoneshwa kwenye maonyesho hayo, 600 kati yake vikiwa ni vile vilivyochukiliwa na wanajeshi wa Kisovieti nchini Ujerumani.

Madai ya Ujerumani

Ujerumani imekuwa ikitaka kurejeshewa kwa kile inachokiita "kazi za sanaa zilizochukuliwa ngawira", ikirejea kwenye sheria za kimataifa, lakini Urusi imekataa, ikisema kwamba hazina hizo zilipatikana baada ya kupotea kwa roho kadhaa za wanajeshi wa Kisovieti.

Kikosi cha wanajeshi wa Kisovieti kwenye Mto Elbe wa Ujerumani tarehe 25 Aprili 1945.
Kikosi cha wanajeshi wa Kisovieti kwenye Mto Elbe wa Ujerumani tarehe 25 Aprili 1945.Picha: picture-alliance/akg-images/RIA Nowosti

Taarifa za kufutwa kwa hotuba hizo za ufunguzi kutoka kwa viongozi wote wawili, zilikuja muda mchache tu kabla ya Merkel kupanda ndege kuelekea Saint Petersburg. Shirika la habari la Ujerumani (dpa) limevinukuu vyanzo vilivyo karibu na Kansela Merkel vikisema kwamba sababu ya kufutwa kwa hotuba hizo, ni namna ambavyo Merkel angelizitaja hazina hizo kwenye hotuba yake.

Hata hivyo, bado mkutano wa pamoja na waandishi wa habari kati ya Merkel na Putin, bado utafanyika kama ulivyopangwa.

Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Ujerumani unaambatana na Kansela Merkel kwenye mkutano huo wa kimataifa.

Mji wa Saint Petersburg ni wa pili kwa ukubwa nchini Urusi. Mwakani, mji huo utaadhimisha mwaka wa 70 tangu kumalizika kwa kuzingirwa kwa  kikosi cha Leningrad na wanajeshi wa Ujerumani kwenye Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, ambapo wakaazi wake wengi walikufa kwa njaa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman