Ziara ya Ahmedinejad Lebanon yamalizika kwa hisia mchanganyiko | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ziara ya Ahmedinejad Lebanon yamalizika kwa hisia mchanganyiko

Rais Mahmoud Ahmedinejad wa Iran amekamilisha ziara yake yenye utata nchini Lebanon, lakini vyombo vya habari nchini humo vinasema ziara hiyo imewacha ujumbe mzito kwa Israel na Marekani

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, akiwapungia mkono wafuasi wake katika maandamano yaliyoandaliwa na Hizbullah kwenye mji wa karibu na mpaka wa Israel wa Bint Jbeil, tarehe 14 Oktoba 2010. (AP Photo/Hussein Malla)

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, akiwapungia mkono wafuasi wake katika maandamano yaliyoandaliwa na Hizbullah kwenye mji wa karibu na mpaka wa Israel wa Bint Jbeil, tarehe 14 Oktoba 2010. (AP Photo/Hussein Malla)

Ziara ya Rais wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran, Mahmoud Ahmedinejad, nchini Lebanon imemalizika kama ilivyoanza - kwa mchanganyiko wa hisia za kuilaani na kuinga mkono.

Kwa upande mmoja, vyombo vya habari vya Kimagharibi na waungaji mkono wao ndani ya Lebanon yenyewe, wameichorea taswira ya kuionesha kwamba ziara hiyo haikuwa chochote zaidi ya ugeni wa kiongozi huyo kwa kundi la Hizbullah tu, ambalo lenyewe linatambuliwa na Israel na Marekani kama kundi la kigaidi.

Kwa upande mwengine, waungaji mkono wa kiongozi huyo, miongoni mwa viongozi wa kisiasa na wananchi wa kawaida nchini humo, na ambao hata si wafuasi wa madhehebu ya Shia wala wa kundi la Hizbullah, wanaiona taswira halisi ya Ahmedinejad kuwa ni kubwa na ya kuheshimika nchini mwao.

Maputo yenye rangi za weupe na buluu ambazo ni rangi za bendera ya Israel yakiwa yamewekwa na wanaharakati nchi Israel nyuma tu ya kijiji cha Kfar Kila ambapo Rais Mahmoud Ahmedinejad alikuwa anatembelea jana 14 Oktoba 2010. (AP Photo/Ariel Schalit)

Maputo yenye rangi za weupe na buluu ambazo ni rangi za bendera ya Israel yakiwa yamewekwa na wanaharakati nchi Israel nyuma tu ya kijiji cha Kfar Kila ambapo Rais Mahmoud Ahmedinejad alikuwa anatembelea jana 14 Oktoba 2010. (AP Photo/Ariel Schalit)

"Ziara ya Mahmoud Ahmedinejad, Rais wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran kwetu ni kitu kitukufu sana kwetu watu wa Lebanon. Huyu ni kiongozi ambaye daima amewaunga mkono Wapalestina na Waarabu wote katika dhiki yao chini ya ukaliaji wa Israel." Anasema mzee mmoja katika mitaa ya mji wa Beirut.

Tahariri katika gazeti la leo (15 Oktoba 2010) la Anwar la nchini humo, inasema ziara hii inakusudia kuwaambia Wamarekani kwamba "Ikiwa mutaitenga Iran, basi Iran itawategeni Lebanon na kwengineko. Ujumbe ni kuwa kama Washington inataka suluhisho katika eneo hili, basi lazima ikapige hodi kwenye mlango wa Iran."

Lakini tangu mwanzo, Marekani na Israel zilishaweka wazi msimamo wao kwa ziara hii. Msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje ya Israel, Yigal Palmor, alifika umbali wa kuishambulia Lebanon kwa maneno, kwamba kumualika na kumpa mapokezi iliyompa Ahmedinejad kumethibitisha namna nchi hiyo ilivyo kibaraka wa Iran katika eneo la Mashariki ya Kati.

"Udhibiti wa Iran kwa Lebanon kupitia kibaraka wake Hizbullah umeharibu fursa ya kupata amani, umeifanya Lebanon kuwa dola inayotumiliwa na Iran na kituo kikuu cha ugaidi na ukosefu wa utulivu kwenye eneo hili." Amesema Palmor.

Maoni kama haya ndiyo pia yanayotolewa na Marekani. Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Philip Crowley, amesema kwamba ziara ya Rais Ahmedinejad nchini Lebanon, hasa katika eneo la Kusini linalodhibitiwa na kundi la Hizbullah, inaonesha wazi kwamba Iran inajaribu kutumia ushawishi wake kulifanya eneo hili lisiwe na utulivu.

Kwa vyovyote vile, ziara ya Rais Ahmedinejad nchini Lebanon imeacha ujumbe mzito kwa siasa za Mashariki ya Kati. Udhibiti wa Israel katika eneo hili umeingizwa kwenye mtihani mkubwa.

Kumbukumbu za vita vya mwezi Machi 2006 baina yake na Lebanon, ambavyo Hizbullah ilipambana hadi pale majeshi ya Israel yalipoamriwa kujiondoa kwenye ardhi ya Kusini ya Lebanon, zina mwangwi mbaya sana. Na kama kuna chochote, basi ziara hii imeukumbushia mwangwi huo.

Na huenda ukawa ni mwangwi huu ambao kiongozi wa Hizbullah, Hassan Nasrallah, angelitaka uendelee kusikika hata baada ya Rais Ahmedinejad kupanda ndege na kurudi alikotoka. Ndio maana akampa kiogozi huyo zawadi ya kombora la Israel lililotekwa na wapiganaji wake wakati wa vita hivyo vya Machi 2006.

Kwa upande mmoja, zawadi hii ilikuwa ni ishara ya utiifu na shukrani zake kwa Rais Ahmedinejad binafsi kwa kuwaunga mkono kihali na mali, Hizbullah; na, kwa upande mwengine, ni shara ya ushindi na uchokozi dhidi ya Israel inayoliangalia kundi hilo kama adui wake namba moja katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

 • Tarehe 15.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pesp
 • Tarehe 15.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pesp
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com