Mitchell ziarani Lebanon. | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.09.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mitchell ziarani Lebanon.

Mjumbe maalumu wa Marekani anayehusika na Mashariki ya Kati yuko mjini Beirut kwa ajili ya kukutana leo na Rais wa Lebanon, Michel Sleiman, kama sehemu ya juhudi za Marekani kuhakikisha kwamba amani inafanikiwa.

default

Mjumbe maalumu wa Marekani anayeshughulikia mashariki ya kati George Mitchell.

Mjumbe huyo Marekani anayeshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati, George Mitchell, amewasili nchini Lebanon jana jioni akitokea Syria, na kufanya mazungumzo kwanza na spika wa bunge la nchi hiyo, Nabih Beri, na maafisa kutoka katika ofisi ya Waziri mkuu wa nchi hiyo, Saad Hariri.

Hata hivyo, hakutoa taaarifa yoyote kuhusiana na mazungumzo yao hayo.

Akiwa nchini Syria, Bwana Mitchell alikutana na Rais wa nchi hiyo, Bashar al Assad, na kusema kuwa kwa  Marekani makubaliano hayo ya kupatikana kwa amani yanamaanisha makubaliano kati ya Israel na Wapalestina, kati ya Israel na Syria, na ni makubaliano pia kati ya Israel na Lebanon na pia ni kurudisha tena uhusiano wa kawaida kati ya Israel na majirani zake.

Aidha alifahamisha kwamba uzito wa Marekani katika kufikia muafaka kati ya Israel na Palestina hautageuza msisitizo wa Marekani kutaka kufikiwawa  mapatano kati ya Israel na Syria.

Kimsingi, Lebanon na Syria  bado ziko vitani na Israel, na kwamba Marekani ina matumaini ya kuyashawishi mataifa yote hayo kuingia katika mazungumzo ya amani na taifa hilo la Kiyahudi na kuunga mkono mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina.

Wakati mjumbe huyo wa Marekani katika mashariki ya kati, akiwa nchini Lebanon leo, jana Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Marekani, Bibi Hilary Clinton, alikamilisha mazungumzo yake ya siku tatu na viongozi wa Israel na Palestina bila ya kufikia makubaliano yoyote juu ya kusitishwa kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi katika ukingo wa magharibi.

Wapalestina wamesisitiza msimamo wao wa kujitoa katika mazungumzo hayo iwapo ujenzi huo utaanza tena baada ya muda wa kuruhusu ujenzi huo utakapomalizika tarehe 30 ya mwezi huu wa Septemba. Israel imesisistiza kuwa haitaongeza muda huo.

Wakati mazungumzo ya ana kwa ana ya amani kati ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, yakiingia katika duru ya pili, wanajeshi wa Israel wamemuua kwa kumpiga risasi mwanachama mwandamizi katika kundi la wapiganaji la Hamas, katika shambulio walilolifanya katika mji wa Tilkarm, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Msemaji wa jeshi la Israel amesema tukio hilo limetokea baada ya wanajeshi wa nchi hiyo kufika katika nyumba ya Iyad Assad Ahmed Abu Salamia, ambaye aliwahi kufungwa awali kwa nia ya kutaka kumkamata, lakini badala yake aliwakimbilia na ndipo walipomfyatulia risasi.

Uchunguzi zaidi unafanywa juu ya tukio hilo.

Mwandishi: Nyanza, Halima/DPA/Reuters

Mhariri:  Miraji Othman

 • Tarehe 17.09.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PERn
 • Tarehe 17.09.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PERn
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com