Ziada ya bajeti Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ziada ya bajeti Ujerumani

Kwa mara ya kwanza tangu muugano kati ya Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi miaka 17 iliyopita, nchi hiyo imeweza kuwa na ziada katika bajeti yake. Kulingana na idara ya takwimu ya Ujerumani, sababu yake ni kuongezeka kwa mapato ya serikali kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.

Uchumi unaendelea kuboreka nchini Ujerumani

Uchumi unaendelea kuboreka nchini Ujerumani

Kulingana na idara ya takwimu ya Ujeramani, serikali ya shirikisho ya Ujerumani, serikali za majimbo na wilaya zimeweza kuwa na ziada ya bajeti ya Euro Billioni 1.2 ambazo ni sawa na asilimia 0.1 ya mapato ya taifa. Takwimu hizo zimechapishwa pamoja na nyaraka nyingine kutoka sekta ya biashara ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa katika kukua kwa uchumi wa Ujerumani.

Volker Kauder ni mwenyekiti wa kundi la vyama ndugu vya kihafidhina CDU/CSU, naye anasema: “Kuwa na ziada ya bajeti katika miezi sita iliyopita kweli ni habari nzuri kwetu. Lakini mahesabu yatakamilishwa mwishoni mwa mwaka tu. Bado hatujatatua shida yetu ya bajeti. Bado tulilazimika kuchukua mikopo, na kila mwaka tunalipa Euro Billioni 30 ikiwa ni riba. Lakini tunafanya bidii kubwa kufikia lengo letu ambalo ni kutolazimika tena kuchukua mikopo kuanzia mwaka 2011.”

Licha ya ziada hiyo, hakutakuwa na upungufu wa kodi kwa wateja na makampuni. Haya aliyasema waziri wa fedha, Peer Steinbrück, akikumbusha juu ya mzigo mkubwa wa deni. Kwa hivyo, kodi haitapunguzwa hadi mwisho wa muda wa serikali hiyo kuwa madarakani mwaka 2009. Kwenye gazeti moja maarufu, waziri Steinbrück ananukuliwa akisema: Yule anayetaka kodi zipunguzwe anaendelea moja kwa moja na sera hizo hizo ambazo zimesababisha mzigo wa deni kukua kupita kiasi.

Waziri Steinbrück wa chama cha Social Demokrats anaungwa mkono na wenzake wataalamu wa bajeti wa chama cha Kihafidhina ambao walisema pia, kodi zitapunguzwa tu pindi deni litakapomalizika. Bado kuna ukosefu wa Euro Billioni 30 kila mwaka ambapo serikali inalazimika kukopa.

Wanaodai kodi zipunguzwe ni wa chama cha Liberali na vilevile wa jumuiya ya walipa kodi wakisema kuwa wananchi wanapaswa kunufaika na kurudishwa fedha walizozilipa kwa muda mrefu.

Tangu muungano wa Ujerumani, serikali inatumia fedha zaidi kuliko inazopata. Mnamo mwaka 2000 peke yake mapato yalikuwa makubwa kutokana na kuuza leseni za UMTS, aina ya kisasa ya mawasiliano ya simu za mkononi. Mwaka jana upungufu wa bajeti ulifika Euro Billioni 23. Kwa muda wa miaka mitatu, kuanzia 2002 hadi 2005 Ujerumani ilivunja makubaliano ya Umoja wa Ulaya juu ya upungufu wa bajeti. Tangu mwaka wa 2005 uchumi wa Ujerumani umeboreka.

Ndiyo sababu, halmashauri ya Umoja wa Ulaya imepokea vizuri habari juu ya ziada ya bajeti nchini Ujerumani. Hata hivyo, msemaji wa kamishna anayehusika na sarafu alisisitiza kuwa Ujerumani isisimamishe juhudi zake za kuweka sawa bajeti na kupunguza deni zake.

 • Tarehe 23.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH9C
 • Tarehe 23.08.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH9C
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com