Yaliyomo katika magazeti ya Ujerumani hii leo | Magazetini | DW | 22.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Yaliyomo katika magazeti ya Ujerumani hii leo

Mada zinazozingatiwa kwenye kurasa za wahariri ni tofauti: Mkutano kati ya Jimmy Carter na kundi la Hamas, uchaguzi wa mapema Marekani na uchaguzi wa Paraguay.

default

Hivi jana kulifanywa mazungumzo kati ya rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter, na kundi la Hamas. Gazeti la “Märkische Allgemeine” linatathmini hivi mkutano huu:


“Rais wa zamani Carter amechukua hatua isiyo ya kawaida kwa kukutana na wajumbe wa kundi la kiislamu la Hamas. Kundi hili linalokataa kulitambua taifa la Israel na ambalo limefanya mashambulio mengi ya kigaidi halikubaliwi kama mshirika wa mazungumzo huko Washington, Tel Aviv au Brussels. Kwa hivyo, hasira kuelekea safari hii ya Jimmy Carter ilikuwa kubwa. Lakini kwa kukataa mazungumzo, mzozo huu mgumu hauwezi kutatuliwa. Tishio kutoka kwa nje halisaidii kuendelea mbele.”


Mada nyingine bila shaka ni matarajio mbele ya uchaguzi mwingine wa kuchagua wagombea wa urais utakaofanyika leo hii katika mkoa wa Pennsylvania, Marekani. Mhariri wa “Badische Zeitung” amechambua nafasi za Barack Obama kushinda katika uchaguzi huu wa mapema na ameandika hivi:

“Katika enzi hii ya mtandao wa Internet inachukua muda mfupi tu kupata umaarufu mkubwa. Barack Obama lakini anapaswa kuwa na uangalifu na kutotegemea mno sifa yake ambayo inamfanya kama mkombozi mwenye kuboresha hali ya watu wengi. Na hata watu duniani kote wanapaswa kutodanganywa na kampeni hiyo kubwa. Kwani, ikiwa Obama kweli atachaguliwa rais, yeye pia atatetea maslahi ya Marekani ambayo mara nyingi hayaendi sambamba na maslahi ya mataifa ya Ulaya au mengine.”

Tuendelee na siasa huko Amerika ya Kusini ambapo askofu wa zamani Fernando Lugo alishinda uchaguzi wa rais. Gazeti la “Dithmarscher Landeszeitung” linaeleza hivi juu ya tukio hili:


“Uchaguzi huu wa Paraguay unaonyesha kwamba mwenendo uliopo Amerika ya Kusini unaendelea. Hata ikiwa mshindi huyu anatetea mrengo wa kati, bado ni wazi kwamba Paraguay, sawa na nchi nyingine kubwa kama Mexiko au Columbia inaelekea mrengo wa shoto. Juu ya hayo lakini, kuna sababu nyingine uchaguzi huu kuwa wa kihistoria, yaani kwamba wapinzani wa Lugo walikubali kushindwa. Wakati serikali nyingine ya mabavu inabadilishwa kwa njia ya amani na kidemokrasia, washindi wengine walio wa mrengo wa kushoto wanageuka kuwa viongozi wakali.”


Na kwa mchango wa mwisho katika udondozi wa leo tubakie katika suala la Paraguay na tusikie gazeti la “Lausitzer Rundschau” liliandikaje:


“Katika muda wa miaka miwili tu, askofu wa zamani Fernando Lugo ameweza kupanda daraja na kuchukua cheo cha urais nchini Paraguay. Hii ni ishara vile wananchi walivyochoka na sera mbaya na hali ya kujiamini mno ya chama cha Colorado kilichotawala nchi hiyo kwa kipindi cha miaka 61. Raisi mpya Lugo anaangaliwa kuwa ni mkombozi ambaye anaweza kuiondolea Paraguay matatizo yake makubwa kama maradhi, uhamiaji wa watu wengi kukimbilia nchi za nje, uchumi unaoporomoka na kiwango kikubwa cha rushwa.”

 • Tarehe 22.04.2008
 • Mwandishi Dreyer, Maja
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DmEQ
 • Tarehe 22.04.2008
 • Mwandishi Dreyer, Maja
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DmEQ