1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaonesha kutofautiana na mataifa makubwa duniani

5 Septemba 2023

Uamuzi wa Rais wa China Xi Jinping kughairi kuhudhuria mkutano wa nchi zilizostawi kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi za G20, inadhihirisha kuharibika kwa uhusiano kati ya Beijing na mataifa mengine makubwa duniani.

https://p.dw.com/p/4Vz8L
Südafrika Johannesburg | BRICS-Gipfel | Pressekonferenz
Picha: Sergei Bobylev/dpa/picture alliance

Wizara ya mambo ya nje ya Beijing imesema kwamba Waziri Mkuu Li Qiang ataungana na viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa zaidi duniani mjini New Delhi wikendi hii, na kuthibitisha kutokuwepo kwa Xi. Hata hivyo hakuna sababu iliyotolewa kwa nini Xi hatahudhuria mkutano huo, ambao hajawahi kuukosa tangu aingie madarakani, isipokuwa ulioandaliwa mjini Roma mnamo 2021 ambao alishiriki kwa njia ya video kutokana na vizuizi vya janga la Uviko.

Kukosekana kwake katika mkutano huu kunaibua tofauti kubwa hasa baada ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa nchi zinazoibukia kiuchumi wa BRICS nchini Afrika Kusini mwezi uliopita. Xi alikuwa mstari wa mbele wakati muungano huo ulipokubaliana kuongeza wanachama sita wapya katika kile alichokiita mafanikio ya "kihistoria".

Kulingana na Steve Tsang, mkurugenzi wa Taasisi ya SOAS China, katika Chuo Kikuu cha London, Msisitizo wa kuimarisha uhusiano na ulimwengu unaoendelea unaonyesha juhudi za Beijing katika kile alichokitaja kama "kuunda njia mbadala kwa utaratibu wa kimataifa wa kiliberali unaotawaliwa na Marekani tangu mwisho wa Vita vya Pili vya Dunia."

Tsang ameongezea kwamba mkutano wa G20 sio kitu ambacho China inaweza kukihodhi.Na  kwa hivyo suala hilo haliwezi kupewa nafasi kubwa.

Kuharibika kwa uhusiano kati ya China na mataifa ya Magharibi.

Indien G20 Gipfel l Australischer Finanzminister Jim Chalmers
Waziri wa Uchumi wa Australia Jim Chalmers akiwa katika mkutano wa G 20 wa 18.07.2023Picha: Ajit Solanki/AP/picture-alliance

Kutohudhuria mkutano wa mwaka huu wa G20 pia kunadidimiza matumaini ya kuimarishwa kwa uhusiano kati ya China na mataifa ya Magharibi yenye nguvu. Huku wachambuzi wakihoji kwamba uamuzi wa Xi kutohudhuria mkutano huo huenda umetokana na mgogoro wa muda mrefu kati ya China na mwenyeji wa mkutano wa mwaka huu India.

Beijing na New Delhi wamekuwa na mzozo wa mpaka kwa miongo kadhaa na rabsha mbaya zimezuka kwenye mpaka mkubwa wa Himalaya katika miaka ya hivi karibuni. China pia haikufurahia uanachama wa India wa kile kiitwacho Quad, yaani ushirikiano wa mkakati wa kiusalama wa mataifa manne,ambayo  Australia, India, Japan na Marekani,  Beijing inauona uwanachama wa India katika kundi hilo ni kama jitihada za kuzuia ushawishi wake barani Asia.

Ishara ya upinzani wa India na China.

Shi Yinhong, profesa wa uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu cha Renmin cha Beijing, amesema India pia hivi karibuni imeonyesha "upinzani mkubwa kwa China kudai umiliki wa eneo la Bahari ya Kusini mwa China pamoja na kuongeza marufuku au vizuizi vikali kwa mauzo ya bidhaa za teknolojia za China na uwekezaji wa moja kwa moja".

Kulikuwa na matarajio kwamba Xi angeweza kutumia mktano wa G20 kukutana na Rais Joe Biden, hasa baada ya rais huyo wa Marekani wiki iliyopita kusema kwamba "atasikitika" ikiwa kiongozi huyo wa China hatohudhuria.

Tofauti ya serikali za Beijing na Washington.

Beijing na Washington zimezozana katika miaka ya hivi karibuni kuhusu masuala mbalimbali, kuanzia biashara hadi teknolojia na haki za binadamu. Chama cha Kikomunisti cha China mara chache hufichua habari kuhusu viongozi wakuu lakini usiri wake unaonekana kugonga vichwa vya habari mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni.

Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje Qin Gang aliondolewa ghafla katika wadhifa wake mwezi Julai na tangu wakati huo hajaonekana hadharani. Vile vile Xi alishindwa kutoa hotuba iliyopangwa katika mkutano wa kilele wa BRICS, badala yake akamtuma waziri wa biashara kuisoma kwa niaba yake.

Soma zaidi: Mawaziri wa Mambo ya Nje na Maendeleo wa nchi za G20 wakutana nchini Italia.

Tsang, wa SOAS, alisema kuna uwezekano kwamba Xi, ambaye alitimiza miaka 70 mwaka huu, huenda kuwa ana matatizo ya kiafya na mwanadiplomasia mmoja kutoka kundi la G20 anadhani kwamba huenda rais huyo wa China anaepuka maswali magumu ya kwanini anakataa kuilaani Urusi kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.

Chanzo: AFP