1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ziarani China

8 Desemba 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul amewasili China Jumatatu kwa ziara yake ya kwanza nchini humo.

https://p.dw.com/p/54ux9
Beijing | Johann Wadephul akisalimiana na Wang Wentao, Waziri wa Biashara wa China
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Johann Wadephul akisalimiana na Wang Wentao, Waziri wa Biashara wa China mjini BeijingPicha: Soeren Stache/dpa/picture alliance

Ziara hiyo inafanyika katika wakati ambapo Ujerumani inaonekana kuimarisha msimamo wake dhidi ya China hasa kuhusu migogoro ya kibiashara na ile ya siasa za kilimwengu sambamba na misimamo ya washirika wake wa Ulaya.

Wadephul amekutana na mwenzake wa China, pamoja na waziri wa biashara na baadaye atakutana na mkuu wa idara ya mahusiano ya kimataifa wa Chama cha Kikomunisti. Safari hii ya Wadephul iliyokuwa ifanyike mwezi Oktoba mwaka huu, iliahirishwa kufuatia mivutano na inaandaa ziara ya Kansela wa Ujerumani  Friedrich Merz  hapo mwakani.

Mkutano wa Beijing utagubikwa na masuala ya uhusiano wa kiuchumi kati ya nchi zenye uchumi mkubwa barani Ulaya na Asia huku siku ya Jumanne, Wadephul akiutembelea mji wa kusini mwa Guangzhou ambao ni kitovu cha viwanda. Mwezi uliopita, Ujerumani iliunda kamati ya wataalamu ili kulishauri Bunge kuhusu uhusiano wa kibiashara na China, ikiwa ni sehemu ya msukumo wa kupunguza utegemezi kwa China.