Watuareg wa Mali na Niger waweka chini silaha | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.10.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Watuareg wa Mali na Niger waweka chini silaha

Mapatano ya amani ya Watuareg huko Mali na Niger

default

Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, ambaye pia ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, AU, akizungukwa na bendera za nchi za Afrika

Mali na Niger zimekubaliana juu ya mapatano ya amani ya jumla pamoja na makundi ya kabila la Watuareg ambapo kwamba wapiganaji wao 1,100 wameshaweka chini silaha zao. Hayo yamesemwa na kiongozi wa Libya, Mumammar Gaddafi, ambaye ameyasimamia mapatano hayo..

Watuareg ambao ni watu wa kabila lenye kutangatanga walianzisha uasi katika Jangwa la Sahara katika miaka ya sitini na tisini, na wakarejea tena na uasi tangu mwaka 2007 dhidi ya serekali ya Niger na ile ya nchi jirani ya Mali, hali ambayo imezidisha kukosekana utulivu katika eneo hilo ambako pia matawi ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaida yanafanya harakati zao. Tawi la al-Qaida katika Afrika Kaskazini limezidisha hali ya kukosekana usalama katika eneo hilo ambako makampuni ya kimataifa, kama vile lile la Kifaransa, Areva, na la Kanada, Cameco, yanafanya shughuli zao.

Kanali Muammar Gaddafi alisema jana usiku kwamba saa hiyo ya jana ilikuwa ya kihistoria na yenye umuhimu kwa vile ndugu zao wa Ki-Tuareg katika Mali na Niger wameamuwa kufikia amani na kuweka chini silaha zao. Muammar Gaddafi, ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, AU, alikuwa akiwahutubia makamanda wa vyama vya waasi wa Kituareg na wawakilishi wa serekali za Mali na Niger waliokusanyika katika mji wa jangwani wa Sabha ili kutoa kibali kwa mapatano hayo.

Matamshi yake hayo yalitangazwa na shirika rasmi la habari la Libya. Muammar Gaddafi aliweza kusimamia mapatano ya amani kama hayo miaka miwili iliopita, lakini makundi ya Ki-Tuareg yaliojigawa yaliyakana mapatano hayo, yakizilaumu Mali na Niger kwa kushindwa kuyaheshimu makubaliano hayo.

Muammar Gaddafi alisema kila kundi la makundi ya waasi ya WaTuareg limeahidi kutekeleza mapatano hayo ya amani mara hii na serekali kuu huko Niger na Mali zimetuma wawakilishi wao, wakiwemo majenerali wa jeshi, kuhakikisha kuwa wako tayari kuyaheshimu mapatano hayo. Aliongeza kusema kwamba kwa mara ya kwanza hakutakuweko muasi yeyote mwenye silaha atakayebakia milimani huko Mali na Niger na wale waliozowea kuviongoza vyama vya waasi wako pamoja naye, huku akiwataja wakuu watano wa makundi ya waasi wa Ki-Tuareg kutokea Mali na Niger. Muammar Gaddafi alisema hivi sasa kuna wapiganaji 1,100 ambao wameweka chini silaha zao huko Agades, Niger, na wapiganaji hao wanawasikiliza wao hivi sasa na wanangoja kupata amri kutoka kwa Gaddafi awaambie waingie Niger kwa amani.

Hivyo aliwaambia wasonge mbele na waingie Niger kwa amani.

Kanali Muammar Gaddafi alisema Wa-Tuareg wote wanaoishi Niger na Mali na kwengineko katika maeneo ya Afrika chini ya Jangwa la Sahara walikuwa Wa-Libya, lakini alisema anawataka waishi kwa amani kule ambako wamefanya makaazi. Kiongozi huyo wa Libya, ambaye katika siku za nyuma aliwasaidia waasi wa Ki-Tuareg kwa fedha na silaha, aliwahimiza Wa-Tuareg waachane na matumizi ya nguvu na kushughulikia kuendeleza amani na utulivu katika Mali na Niger.

Muammar Gaddafi anataka Waafrika watanzuwe mizozo katika bara lao ili kuyazuwia madola makuu katika kile anachokisema kuwa ni majaribio ya kuchochea kuanza vita zaidi ili madola hayo yaweze kuuza silaha zaidi na kupanua ushawishi wao katika Afrika ilio na utajiri wa mali ghafi.

Mwandishi: Miraji Othman/AFP

Mhariri: Mohammed Abdulrahman

 • Tarehe 08.10.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/K1lv
 • Tarehe 08.10.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/K1lv
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com