1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wataliban hawataongeza muda wa kuhamishwa watu

23 Agosti 2021

Duru kutoka kundi la Taliban zinasema muda wa mwisho wa Agosti 31 wa majeshi ya nchi za Magharibi kuondoka nchini humo hautaongezwa.

https://p.dw.com/p/3zN1R
Afghanistan | Flughafen Kabul | Italienischer Evakuierungsflug
Picha: Ministero Della Difesa/AFP

Haya yanakuja wakati ambapo Uingereza imeirai Marekani kuongeza muda wake wa kuwaondoa watu nchini humo.

Msemaji wa Taliban ametoa kauli hiyo ya kutokubali kuuongeza muda huo ingawa duru zinaarifu hakuna afisa yeyote wa serikali za Magharibi aliyezungumza na wanamgambo hao kuhusiana na muda huo kuongezwa.

Lakini Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson anapanga kumshinikizaRais wa Marekani Joe Biden kuhusiana na suala hilo katika mkutano wa dharura wa nchi saba zilizostawi kiviwanda G7 hapo Jumanne mkutano ambao Uingereza ndiyo iliyouitisha.

USA Washington | Pressekonferenz Joe Biden zu Afghanistan
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Joshua Roberts/REUTERS

Biden hajaondoa uwezekano wa kuongeza muda wa kuwaodoa majeshi

Uingereza inasema bila Marekani, nchi zengine hazitokuwa na budi ila kusitisha juhudi zake za kuwaokoa watu kutoka nchi hiyo ambayo utawala wake umechukuliwa na kundi la Taliban. Biden hajaondoa uwezekano wa kuongeza muda huo ingawa amesema huenda ikawa hakutokuwa na haja ya kufanya hivyo.

"Tazama, tunashirikiana kwa karibu sana G7. Nimezungumza na viongozi wengi wa G7. Nitafanya mkutano nao nafikiri Jumanne na tutalizungumzia suala hilo," alisema Biden.

Rais Biden pia ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na kitisho kinachoweza kutokana na kundi la Dola la Kiislamu mnamo wakati ambapo jeshi la Marekani linapania kuwaondoa raia wa nchi hiyo na marafiki zake.

Karibu raia 400 wa Afghanistan kupewa hifadhi Ulaya

Biden anadai kundi hilo ni hasimu wa Taliban na kadri wanajeshi wa Marekani wanavyozidi kusalia nchini humo ndivyo uwezekano wa Dola la Kiislamu kuwashambulia wanajeshi wa Marekani na raia wasio na hatia katika uwanja wa ndege wa Hamid Karzai unavyozidi kuongezeka.

Maelfu ya Waafghan wanapanga kuondoka nchini humo

Wakati huo huo mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell anasema karibu raia 400 wa Afghanistan waliokuwa wanafanya kazi na umoja huo watapewa hifadhi Ulaya. Borrell anasema kwa sasa wanapelekwa Uhispania kufanyiwa vipimo na kisha kupelekwa katika nchi tofauti za Ulaya zilizo tayari kuwapa vibali vya kuishi nchini mwao.

Hayo yakiarifiwa jeshi la Ujerumani linasema kumeshuhudiwa makabiliano ya risasi katika uwanja wa ndege wa Kabul mapema Jumatatu kati ya maafisa wa usalama wa Afghanistan na wavamizi wasiojulikana.

Katika ujumbe ulioandikwa katika ukurasa wa twitter jeshi hilo limesema mwanajeshi mmoja wa Afghanistan ameuwawa na wengine watatu kujeruhiwa katika tukio hilo la mapema.

Kundi la Taliban nalo linasema wapiganaji wake wamewazunguka wanajeshi wanaowapinga katika bonde la Panjshir ila wanataka kufanya majadiliano nao badala ya kupigana nao.