Washington: Fischer anaunga mkono mpango wa Marekani
18 Novemba 2003Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani, Joschka Fischer, anaunga mkono mpango wa Marekani wa kuwakabidhi haraka Wairak hatima ya nchi yao. Amesema kuwa hiyo ni hatua inayofaa na inayopaswa kuungwa mkono. Wakati wa mazungumzo yake na Waziri mwenzake Colin Powell na Mshauri wa Usalama wa Rais Bush, Condoleezza Rice mjini Washington, ametoa mwito kwa Umoja wa Mataifa kushirikishwa kwa dhati katika mwenendo huo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, amesema kuwa atauchunguza kwa makini sana mpango huo wa Marekani. Kwa mujibu wa serikali ya Rais Bush, hadi ifikapo katikati ya mwaka ujao kutakuwa na serikali ya mpito mjini Baghdad itakayochukua mahali pa Baraza tawala na Utawala wa kiraia wa Marekani. Ikulu ya Marekani imetilia mkazo hata hivyo kwa kusema kuwa Wanajeshi wake wataendelea kubakia Irak hata baada ya serikali ya mpito kuteuliwa.