Wapalestina waitaka jumuiya ya kimataifa imshinikize Netanyahu | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.06.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Wapalestina waitaka jumuiya ya kimataifa imshinikize Netanyahu

Syria yaikosoa vikali hotuba ya Netanyahu

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu

Wapalestina wamekasirishwa na hotuba ya waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huku Syria ikiieleza kuwa ya kibaguzi na uchochezi. Umoja wa Ulaya na Marekani kwa upande wao zimempongeza Netanyahu zikisema amechukua hatua inayofaa kuelekea suluhisho la mzozo wa Mashariki ya Kati.

Waziri mkuu wa Jamhuri ya Cheki, Jan Kohout, ameisifu hotuba ya waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akisema ni hatua itakayosaidia katika kuutanzua mzozo wa Mashariki ya Kati. Akizungumza hii leo mjini Luxembourg kiongozi huyo amesema kuna vipengee kadhaa vinavyohitaji kuchambuliwa katika hotuba ya Netanyahu, lakini amekubali taifa la Palestina.

Waziri mkuu wa Sweden Carl Bildt, ambaye nchi yake itachukua urais wa Umoja wa Ulaya kuanzia Julai mosi mwaka huu, pia amempongeza bwana Netanyahu.

Chini ya shinikizo la Marekani waziri mkuu Netanyahu ameidhinisha kwa mara ya kwanza kuundwa kwa taifa huru la Palestina ambalo halitakuwa na silaha, iwapo Wapalestina waitambua Israel kuwa taifa la kiyahudi. Katika hotuba yake hiyo, Netanyahu amefutilia mbali uwezekano wa kusitisha ujenzi wa makazi ya walowezi wa kiyahudi kama ilivyotakiwa na Marekani.

Msemaji wa ikulu ya Marekani, Robert Gibbs amesema rais wa Marekani Barack Obama ameikaribisha hotuba ya Netanyahu akisema anaamini suluhisho la mzozo baina ya Israel na Palestina linaweza na sharti lihakikishe usalama wa Israel na kutimizwa kwa lengo la kuundwa dola huru la Palestina ambayo ni haki msingi ya Wapalestina.

Ujerumani nayo pia imeipongeza hotuba ya Netanyahu. Msemaji wa serikali ya Ujerumani, Thomas Steg amesema leo kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Berlin kwamba inatia moyo kwa kiongozi huyo kukubali suluhisho la mataifa mawili, jambo ambalo ni la umuhimu mkubwa katika kuanza kwa mazungumzo ya kusaka amani ya Mashariki ya Kati.

Huku dola kuu zikiipongeza hotuba ya Netanyahu, Wapalestina wamekasirika na kundi la Hamas ambalo sasa limekamilisha miaka miwili tangu lilipoudhibiti Ukanda wa Gaza, limeieleza kuwa nadharia ya kibaguzi na uchochezi.

Rafiq al Hussein, mpambe wa rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas, anasema "Nadhani alichokisema Netanyahu ni kwamba Wapalestina hawatakuwa na taifa lao. Ameweka masharti ambayo hayakubaliki. Nadhani kutumia hotuba yake ametangaza vita sio tu dhidi ya Wapalestina, bali ulimwengu mzima."

Wapalestina sasa wanaitegemea jumuiya ya kimataifa kumshinikiza Netanyahu akubali kuundwa taifa la Palestina. Rais wa Lebanon, Michel Sleiman, ameihimiza jumuiya ya kimataifa kuishinikiza Israel na kusema hotuba hiyo inatakiwa kuwaunganisha viongozi wa kiarabu wawe macho zaidi.

Syria imeikosoa vikali hotuba ya Netanyahu ikisema inahatarisha juhudi zote za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati. Gazeti la Al Baath linalotumiwa kama chombo na chama tawala nchini Syria, limesema waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, amethibitisha kuwa anapinga mpango wa nchi za kiarabu kuhusu amani ya kudumu pamoja na juhudi zote na maazimio ya awali ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais wa Misri Hosni Mubarak naye pia amesema matamshi ya Netanyahu yanayazika matumaini ya kupatikana amani kati huko Mashariki ya Kati. Urusi nayo imeelezea wasiwasi wake kuhusu hotuba ya Netanyahu. Wizara ya mamboy a kigeniy a nchi hiyo imesema ingawa hotuba hiyo inaonyesha Israel iko tayari kuanza mdahalo, haifungui mlango wa kulisuluhisha tatizo kati ya Israel na Wapalestina.

 • Tarehe 15.06.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IACo
 • Tarehe 15.06.2009
 • Mwandishi Charo Josephat
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/IACo
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com