Wanawake wachangamkia kusakata gozi uwanjani Ujerumani. | Michezo | DW | 23.05.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Wanawake wachangamkia kusakata gozi uwanjani Ujerumani.

Kabumbu sio mchezo wa wanawake hiyo ni kauli iliyotolewa hapo mwaka 1955 na aliyekuwa rais wakati huo wa Chama cha Soka Ujerumani na kuongeza kwamba suala hilo katu halitopewa uzito.

default

Hiki ndio kikosi cha timu ya soka ya taifa ya wanawake Ujerumani ambao ndio mabingwa wa dunia.

Lakini historia imethibitisha tafauti na kauli hiyo.Hivi sasa kuna wanawake zaidi ya milioni moja wanaocheza soka nchini Ujerumani na kwa mujibu wa takwimu rasmi kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA wanawake milioni 26 wanashiriki katika vyama vya soka duniani kote.

Katu haikuwahi kushuhudiwa kabla wanawake wengi sana kucheza soka nchini Ujerumani.Idadi ya hivi sasa ya wachezaji wananawake 1,002,605 iliothibitisha na Shirikisho la Soka Ujerumani DFB imekaribishwa kwa furaha kubwa na chama cha soka cha wanawake na kupongezwa kuwa ni takwimu muhimu ya uwanachama kwa mwaka 2008.

Profesa wa sayansi ya elimu ya michezo Claudia Kugelmann ameliambia shirika la habari la IPS kwamba wanawake wamekuwa wakishika nafasi wanazostahiki na kuzidi kushika zile zilizokuwa zikihodhiwa na wanaume na kwamba hii ni hatua ya kusonga mbele kwa kuzingatia haki sawa.

Maoni kama hayo anayo Profesa Gertrud Pfister ambaye ana shahada ya udaktari katika sayansi za elimu na saikolojia na ni mtaalamu juu ya historia ya michezo na dhima ya wanawake katika fani hiyo.Pfilster ameliambia shirika la habari la IPS kwamba kuongezeka kwa idadi ya wachezaji soka wa kike kumechangia kupinga taswira ya wanawake kuwa dhaifu na kutengwa katika jamii.

Hata hivyo amesema mara nyingi inakuwa vigumu kutokomeza chuki isio na msingi wa haki licha ya kuwepo ushahidi dhidi ya chuki za aina hiyo kwani anasema hadi hii leo wanaume wanaendelea kutafautisha kati ya kabumbu hasa la wanaume na kabumbu la wanawake.

Mchezaji soka wa kike Annika Leber hivi kariubuni ameliambia gazeti la taifa kwamba akiwa kama mchezaji wa soka anakabiliwa na chuki isiokuwa na msingi kwamba watu wengi humuuliza kwanini ashaukwe juu ya mchezo wa wanaume.

Hildegard Junker mchezaji wa ulinzi naye anasema pia amekuwa akisikia maneno kama vile kwani nini unakimbia hapa na pale nenda ukampikie mumeo na watoto kwani wanasubiri chakula cha jioni.

Kwa kweli wanawake walikuwa wamepigwa marufuku rasmi kucheza kandanda hapo mwaka 1955 kwa hoja wakati huo kwamba wana upungufu wa nguvu za kimwili na kisaikolojia zinazohitajika katika mchezo huo.

Ni mwaka 1970 tu Shirikisho la Soka Ujerumani DBF limeondowa marufuku hiyo kwa sharti kwamba wanawake wacheze wakati wa miezi ya majira ya joto tu.

Zaidi ya miongo miwili imepita kabla ya kutambuliwa kwa mara ya kwanza na Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA Mchuano wa Kombe la Soka Duniani wa Wanawake uliofanyika nchini China hapo mwaka 1991.

Idadi ya wachezaji soka wanawake imekuwa ikiongezeka kwa haraka duniani katika kiwango kupindukia kile cha wanaume.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka FIFA hivi karibuni idadi ya wachezaji wanawake waliojiandikisha kusakata soka imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 50 kati ya mwaka 2000 na mwaka 2006 wakati idadi ya wachezaji wa kiume imeongezeka kwa asilimia 21 tu.

Kwa kuongezea timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini Ujerumani ambayo ndio mabingwa wa dunia ilitetea taji lake kwa mafanikio huko China hapo mwaka 2007 na inawania tena taji hilo wakati wa Michuano ya Kombe la Soka la Dunia kwa Wanawake itayofanyika hapo mwaka 2001 safari hii ikiwa mwenyeji wa mashindano hayo.

Michuano hiyo ya mabingwa wa soka wanawake duniani itafanyika nchini Ujerumani ambapo soka linaonekana kama ni dini.

 • Tarehe 23.05.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E4f2
 • Tarehe 23.05.2008
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/E4f2
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com