1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wakuu wa nchi za afrika washindwa kuafikiana

Tuma Dandi4 Julai 2007

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afria AU wamerejea makwao baada ya kushindwa kufikia muafaka wa kuunda Muungano wa Afrika, katika kilele cha mkutano wa tisa uliofanyika nchini Ghana.

https://p.dw.com/p/CHBg
Rais wa Ghana Bwana John Kufuor
Rais wa Ghana Bwana John KufuorPicha: AP Photo

Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Afria AU wamerejea makwao baada ya kushindwa kufikia muafaka wa kuunda Muungano wa Afrika, katika kilele cha mkutano wa tisa uliofanyika nchini Ghana.

Majadiliano ya kuundwa kwa muungano huo yamegubikwa na totauti kubwa miongoni mwa marais wa nchi za kiafrika, na kuunda makundi mawili.

Kundi la kwanza ni lile linaloongozwa na Rais wa Libya Muammar Gaddafi na Rais wa Senegal Abdoulaye Wade, wanaotaka Muungano huo kusainiwa haraka.

Upande wa pili unaundwa na baadhi ya viongozi kutoka kusini na Mashariki mwa Afrika wanaotaka kuboreshwa kwa uchumi na ushirikiano kati ya nchi na nchi.

Akifunga mkutano huo Rais wa Ghana bwana John Kufuor, amesema maazimio yaliyofikiwa yatapelekwa katika kamati ya Umoja wa Afrika kwa ajili ya maandalizi ya mkutano mwingine utakaofanyika mapema mwaka kesho.

Rais huyo ameongeza kwamba kuundwa kwa muungano wa afrika siyo sera ya kimapinduzi, bali ni ushirikiano ambao kila nchi inapaswa kutia saini baada ya kuridhia mkataba.

Kambi ya rais Muammar Gaddafi wa Libya inataka hadi kufikia mwakani Afrika ianze kuwa na jeshi la pamoja, uchumi mmoja na ushirikiano wa karibu katika masuala ya kisiasa.

Hata hivyo rais Gaddafi na abdoulaye Wade hawakuwepo katika chumba cha mkutano wakati rais wa Ghana bwana John Kufuor akitoa hitimisho la mkutnao huo.

Rais Umaru Yar’adua wa Nigeria ambaye huu ni mkutano wake wa kwanza, ameunga mkono kuwepo kwa ushirikiano wa pamoja, lakini baada ya kuinua maisha ya raia wa kila nchi na baadaye kufanya shirikisho.

Maandalizi ya mkutano ujao yanatarajia kuwa katika sura mbili, ya kwanza itahusu aina gani ya muungano unaohitajika kwa waafrika, wakati ya pili ni kuangalia vyanzo vitakavyofanikisha kuwepo kwa muungano huo.

Awali Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe alisema ikiwa afrika itaunganisha rasilimali zake pamoja, raia watapata nafuu ya maisha, kwa kuwa hawatategemea misaada kutoka mataifa makubwa na mashirika ya fedha yenye masharti makubwa.

Kwa miaka kadhaa sasa serikali ya Zimbabwe inakabiliwa na vikwazo vya uchumi kutoka kwa nchi za magharibi baada ya Rais Mugabe kuanzisha sera ya kutaifisha mashamba ya walowezi wa kizungu, na kuwapa ardhi wananchi ambao hawakuwa nayo.

Wazo la kutaka kuundwa kwa muungano wa afrika linatokana na hisia kwamba umoja wa Afrika umeshindwa kufikia uboreshaji wa maisha ya waafrika kwa kupunguza umaskini, vita, magonjwa na ujinga.

Hatua hiyo pia inaungwa mkono na mwenyekiti wa umoja wa Afrika Bwana Alpha Oumar Konare.

Kiongozi huyo amekaririwa akisema kuwa madhumni yao ni kuona afrika ikiungana pamoja, lakini akakiri kuwa majadiliano bado yana safari ndefu kufikia lengo.

Wapenda maendeleo barani afrika wana hamu ya kuona ndoto hizo zilizoasisiwa na rais wa kwanza wa Ghana marehemu Kwame Nkrumah kuunda muungano wa afrika, zitafikia wapi.