1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wabunge wa Marekani wazuia ufadhili muhimu kwa Haiti

Zainab Aziz
15 Machi 2024

Wabunge wa Marekani wamezuia fedha kwa ajili ya ujumbe wa kimataifa nchini Haiti. Wakati huo huo mpango wa kuunda baraza la serikali ya mpito unasonga mbele lakini viongozi watarajiwa wanakabiliwa na vitisho.

https://p.dw.com/p/4dg4F
Bunge la Marekani
Wabunge ndani ya Bunge la MarekaniPicha: Andrew Harnik/AP Photo/picture alliance

Wabunge wa Marekani wanapinga kuidhinisha fedha kupelekwa nchini Haitiambazo zingelisaidia katika juhudi za kupambana na ongezeko la umwagikaji damu. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilitoa maombi ya dola milioni 40 kwa ajili ya Haiti, lakini wabunge wa chama cha Republican wameweka vigingi. Wabunge hao wameiambia wizara ya mambo ya nje kuwa wanahitaji kupatiwa maelezo zaidi kabla ya kuidhinisha msaada mwingine wa fedha.

Soma Pia:Haiti yajiandaa kwa serikali mpya baada ya Henry kujiuzulu

Hata hivyo watumishi wa Bunge wamesema fedha zinazozuiwa zitatatiza zoezi la kupelekwa polisi wa Kenya nchini Haiti, la sivyo itapasa nchi nyingine ichukue jukumu hilo. Wakati huo huo yamejitokeza mashaka kutokana na Kenya kusema kuwa inasimamisha zeozi la kuwapeleka maafisa wake nchini Haiti baada ya waziri mkuu Ariel Henry, mapema wiki hii kuahidi kujiuzulu baada ya kuundwa baraza la mpito na kupatikana kiongozi wa muda.

Mwaka uliopita Kenya iliahidi kuwapeleka maafisa wake 1000 kuliongoza jeshi la kimataifa nchini Haiti lakini zeozi hilo limekabiliwa na changamoto za mahakamani, aidha Kenya iliomba kulipwa fedha kabla ya kuwapeleka maafisa wake.

Marekani yaahidi kuongeza msaada kwa Haiti

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Andrew Caballero-Reynolds via REUTERS

Wabunge wa Marekani wana mashaka iwapo mahakama nchini Kenya zitaruhusu maafisa wa usalama wa nchi hiyo wapelekwe Haiti. Fedha hizo, milioni 40 zinahitajika kwa ajili ya kulipia gharama zote muhimu za walinda amani. Maafisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani wanaendelea kufanya mazungumzo na wabunge juu ya msada huo. Marekani imeahidi kuongeza msaada hadi dola milioni 300 kwa ajili ya Haiti. Waziri wake wa mambo ya nje Antony Blinken aliyatangaza hayo kwenye mkutano uliofanyika Jamaica mapema wiki hii.

Soma Pia:Waasi wapinga kuwekwa serikali ya mpito nchini Haiti

Wakati huo huo  mpango wa kuunda baraza litakaloendesha serikali ya mpito unasonga mbele baada ya vyama na miungano ya kisiasa kuwasilisha majina kwa wahusika watakaotafuta viongozi wapya wa nchi hiyo. Majina hayo yalikabidhiwa kwa kambi ya kibiashara ya kanda ya Karibik, Caricom, inayo simamia hatua za kufikiwa mpango huo wa kipindi cha mpito.

Na kiongoziwa genge lenye nguvu nchini Haiti Jimmy "Barbeque" Cherizier, ametoa ujumbe wa vitisho unaowalenga viongozi wa kisiasa watakao shiriki katika serikali ya mpito inayokuja. Mbabe huyo alirekodi ujumbe wa dakika saba uliosambazwa hapo jana Alhamisi kupitia jukwaa la WhatsApp.

Soma Pia:Kiongozi wa magenge Haiti aapa kuendelea na mapambano

Mapigano kati ya magenge yameongezeka nchini Haiti kiasi cha kusababisha hali mbaya kwa watu ya kukosekana chakula na pia kusababisha maelfu ya watu kuyakibimbia makaazi yao.

Vyanzo: RTRE/AP/AFP