1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHaiti

Haiti yajiandaa kwa serikali mpya baada ya Henry kujiuzulu

13 Machi 2024

Haiti inajitayarisha kwa serikali mpya siku moja baada ya waziri mkuu Ariel Henry kutangaza kuwa anajiuzulu kufuatia shinikizo lililotokana na kusambaa kwa wimbi la vurugu za magenge ya wahalifu.

https://p.dw.com/p/4dSWt
Machafuko nchini Haiti
Magenge ya wahalifu ikiwemo lile linalofahamika kama G9 yamefanya mfululizo wa mashambulizi yaliyoitikisa Haiti kwa wiki kadhaa. Picha: Odelyn Joseph/AP Photo/picture alliance

Hali kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, inaarifiwa ilikuwa ya utulivu kutwa nzima ya jana baada ya kutolewa tangazo la kujiuzulu Waziri Mkuu Ariel Henry.

Kiongozi huyo alisema atawachia madaraka pale Baraza la Utawala wa mpito likapoundwa na kuanza kazi. Henry bado amekwama kwenye kisiwa jirani cha Puerto Rico baada ya kushindwa kurejea nchini mwake kutokana na wimbi la mashambulizi ya magenge ya uhalifu yaliyokuwa yakimtaka ajiuzulu.

Hivi sasa magenge hayo ndiyo yanadhibiti karibu asilimia 80 ya mji mkuu na barabara muhimu za nchi hiyo. Wafuatiliaji wa siasa za Haiti wameonya kwamba itakuwa vigumu kuitawala nchi hiyo bila kuyashirikisha.

Hapo jana, mmoja ya viongozi wenye nguvu wa magenge hayo ya wahuni, Jimmy Cherizier, maarufu "Barbecue" aliwaambia waandishi habari kwamba lengo lao ni "kuuangusha mfumo mzima wa utawala."

Amewatolea mwito raia wa Haiti kujitokeza mitaani kufanya maandamano kuonesha hasira dhidi ya wale anaosema "wameusababishia mateso umma wa Haiti"

Umma wa Haiti wasema hatma ya nchi yao iko mikononi mwao, siyo mataifa ya kigeni 

Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Karibia, CARICOM, walipokutana mjini Kingston, Jamaica.
Viongozi wa Jumuiya ya Nchi za Karibia, CARICOM, walipokutana mjini Kingston, Jamaica.Picha: Andrew Caballero-Reynolds/AP/picture alliance

Licha ya makundi kuwa ndiyo yalianzisha vurumai ya kumtaka waziri Henry ajiuzulu, nafasi yao katika serikali mpya haikutajwa kokote wakati wa mkutano wa viongozi wa kanda ya Karibia.

Mkutano huo wa siku ya Jumatatu huko Kingston, Jamaica, chini ya mwavuli wa jumuiya ya kanda hiyo inayojulikana kwa kifupi kama CARICOM, ndiyo ulifungua njia ya kujiuzulu kwa Henry na kupendekezwa kuundwa utawala wa mpito.

Hata hivyo sehemu kubwa ya raia wa Haiti hawapendelei tena uamuzi kuhusu hatma ya nchi hiyo kupangwa na mataifa ya kigeni ikiwemo yale ya kanda ya Karibia.

"Ni kweli sisi ni wanachama wa CARICOM lakini ni mara ngapi wamekuja hapa? Kila wakati wameshindwa na hawawezi kutufanyia chochote. Kinachotokea hapa hakiihusu jumuiya ya Caricom, kinatugusa sisi - umma wa Haiti na viongozi wa kisiasa walioshindwa kuihami nchi dhidi ya hali tunayoishuhudia. Sasa hivi inafaa tuchukue wenyewe jukumu la hatma ya nchi yetu. Caricom haijatutendea lolote (watu wa Haiti)", amesema mkaazi mmoja wa mji mkuu, Port-au-Prince. 

Kenya yasitisha kwa muda kupeleka kikosi cha polisi kurejesha utulivu nchini Haiti 

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Haiti, Ariel Henry
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Haiti, Ariel Henry Picha: Prime Minister of the Republic of Haiti via X via REUTERS

Hadi sasa haijafahamika ni lini baraza tawala la mpito litaundwa na kuchukua hatamu za uongozi. Serikali ya Haiti inaongozwa kwa mpito na waziri wa fedha Michele Boisvert na mwenyewe amesema yuko tayari kusaidia kupatikana utawala wa mpya na kuukabidhi madaraka.

Hali hiyo ya kukosekana serikali kamili inaonesha ndiyo imeichochea Kenya kutangaza kusitisha mpango wake wa kutuma polisi kwa kwenda kuisaidia Haiti kurejesha utulivu.

Hayo yametangazwa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Kigeni wa Kenya Koriri Sing´oei. Amesema dhamira ya kutuma askari 1,000 wa nchi hiyo kwenda Haiti imesimamishwa kutokana na mabadiliko yanayotokea ikiwamo kukosekana kwa serikali na kuparaganyika kwa utawala wa sheria.

Kenya ilijitwika dhima ya kuongoza kikosi cha kimataifa kwenda Haiti baada ya kutanua kwa machafuko yanayofanywa na makundi ya wahalifu nchini humo.