Waasi wa Nkunda wapigana na majeshi ya serikali-Umoja wa Mataifa | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Waasi wa Nkunda wapigana na majeshi ya serikali-Umoja wa Mataifa

Umoja wa Mataifa umesema kuwa kiongozi wa waasi wa Kitutsi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Laurent Nkunda anaunga mkono amani katika eneo hilo.

default

Askari wa MONUC.Mmoja wao alijeruhiwa katika mapigano katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo

Hata hivyo Umoja huo umeongeza kuwa kumefanyika mapigano makali mwishoni mwa juma kati ya wapiganaji wa Generali huyo muasi na wanajeshi wa serikali ya Kinshasa katika eneo lililoko masafa ya kilomita 100 kaskazini mwa mji wa Goma.

Maelezo kuhusu mapigano ya jumapili ni finyu.Ila shirika la habari la Ujerumani la DPA linamnukuu msemaji wa jeshi la Umoja wa Mataifa linalolinda amani nchini Kongo Luteni Generali Jean-Paul Dietrich,akisema kuwa kulitokea mapigano makali katika eneo la mji wa Riwindi pamoja na viunga vyake. Mji huo ni mdogo na unapatikana katika ambalo liko umbali wa takriban kilomita 125 kaskazini mwa mji wa Goma. Mji wa Goma ndio mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, mkoa ambao umeshuhudia mapigano ya hivi karibuni sehemu za mashariki mwa nchi hiyo.

Msemaji wa MONUC amelielezea shirika la habari la Ujerumani kuwa mapigano kati ya wapiganaji wa kundi la CNDP la Nkunda na majeshi ya serikali yalianza asubuhi na kumalizika jioni.

Hakuna taarifa za hasara iliopatikana kwa pande zote ila Umoja wa Mataifa unasema kuwa askari wake mmoja aliekuwa katika kituo chao cha karibu kilichonaswa kwenye mapigano. Inasemekana alijeruhiwa kidogo.

Kundi la CNDP linadai kuwa baada ya mapigano hayo sasa linalidhibiti mji wa Rwindi. Msemaji wake amesema kuwa eneo hilo leo ni tulivu baada ya kuwasogeza nyuma wanajeshi wa serikali kwa umbali wa kilomita 15. Hakuna taarifa huru kuthibitisha hilo.

Mapigano hayo yamekuja wakati mjumbe wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa mashariki mwa Kongo,rais wa zamani wa Nigeria,Olusegun Obasanjo kukutana na Laurent Nkunda.

Bw Obasanjo amewambia maripota leo mjini Nairobi kuwa Nkunda alimwambia katika mazungo jana kuwa anataka,miongoni mwa mengine hakikisho la jamii ya kimataifa la vikosi vyake kujumulishwa katika jeshi la serikali. Obasanjo ameongeza kuwa Nkunda hataji lolote ambalo litamfanya yeye pamoja na wapiganaji wake kwenda nje ya nchi, ila kujumuishwa katika jeshi la serikali na hivyo antaka hakikisho la hilo kutoka kwa Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Afrika.

Nkunda anailaumu serikali ya Kinshasa kwa kuwahifadhi Wahuru kutoka rwanda wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya halaiki nchini Rwanda ya mwaka wa 1994.Pia anailaumu serikali kwa kushindwa kuwalinda waTutsi.

Serikali ya Kishasa, kwa upande wake,inasema hatua muhimu kuhusu kuutanzua mgogoro wa Kivu imefikiwa. Kwa mujibu wa mwandishi wa DW wa Kinshasa,waziri wa habari Lambert Mende,amesema kuwa serikali yake imekubaliana na ya Rwanda kuwashirikisha maafisa wa upelelezi wa Kigali katika juhudi za Kinshasa za kuwarejesha makwao wapiganaji wa Kihutu wa kundi la FDLR.

Hata hivyo amefafanua kuwa wanajeshi wa Rwanda hawatahusihswa katika zoezi hilo bali maafisa wa Rwanda watasaidia Kongo kutambua waliko wapiganaji hao. Eneo la Mashariki limekuwa na mapigano ya kila mara na moja wa vyanzo ni wpiganaji wa kihuru ambao Nkunda anadai wanatumiwa na serikali ya Kinshasa kumpiga vita.

Kuhusu amani mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa mgogoro wa Mashariki mwa kongo Olusegun Obasanjo amewambia maripota mjini nairobi kuwa Generali muasi amemuambia kuwa amekubali kusitisha mapigano lakini kwa masharti ya kuwa ikiwa na upande mwingine utayaheshimu.

 • Tarehe 17.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Fwkq
 • Tarehe 17.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Fwkq
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com