1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vya Ujerumani vyakubaliana kuunda serikali mpya

24 Novemba 2021

Vyama vitatu vya Ujerumani vimefikia makubaliano ya kuunda serikali mpya ambayo itamaliza enzi ya Kansela wa muda mrefu Angela Merkel, kulingana na Olaf Scholz, ambaye yuko tayari kuchukua nafasi yake.

https://p.dw.com/p/43QNm
Koalitionsgespräche zwischen SPD, Grünen und FDP in Berlin
Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Chama cha mrengo wa kushoto cha Social Democratic (SPD) kimekuwa kikijadiliana na wanamazingira wa chama cha Kijani na chama kingine kinachopendelea biashara cha Free Democratic (FDP) tangu baada ya matokeo ya uchaguzi wa kitaifa uliofanyika Septemba 26.

Na hatimaye muungano wa vyama hivyo vitatu ambao haujawahi kujaribiwa katika serikali ya kitaifa utachukua nafasi ya serikali ya mseto ya vyama vikubwa vilivyozoeleka kijadi kuongoza serikali.

Soma zaidi: Mazungumzo ya kuunda serikali mpya Ujerumani yamegonga mwamba

Waraka wa mkataba huo wa kuunda serikali mpya ya mseto ulioonekana na shirika la habari la AFP Jumatano, umeonyesha kwamba Chama cha Free Democratic (FDP) kitaendesha wizara ya fedha, sheria, usafiri, masuala ya kidijitali, elimu na utafiti katika serikali inayokuja. Huku chama cha Kijani kitachukua wizara ya mambo ya nje na uchumi na wizara ya ulinzi wa hali ya hewa pamoja na masuala ya familia, mazingira, na kilimo.

Deutschland | Coronavirus | PK Ministerpräsidentenkonferenz
Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani anaemaliza muda wakePicha: Michael Kappeler/AFP/Getty Images

Serikali ijayo ya Ujerumani itaimarisha ushirikiano wa Ulaya

Aidha Olaf Scholz, wa SPD aliye tayari kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani, amesema ataweka mpango wa kukabiliana na ongezeko kubwa la maambukizi ya virusi vya corona nchini. Scholz amewaambia waandishi wa habari kwamba kitaundwa chombo cha wataalamu ambacho kitakuwa kinaishauri serikali kila siku kuhusu janga hilo.

Halikadhalika vyama hivyo vitatu ambavyo vitaunda serikali ijayo ya Ujerumani vitaondoa matumizi ya makaa ya mawe ifikapo 2030, miaka minane mapema kuliko ilivyopangwa hapo awali.

Soma zaidi: Ujerumani: Scholz akubaliana na Kijani, FDP kuanza mazungumzo ya kuunda serikali

Pia wamekubaliana kuimarisha umoja wa kiuchumi na wa sarafu wa bara la Ulaya, kulingana na hati ya muungano iliyoonekana na shirika la habari la Reuters. Scholz pia alisisitiza umuhimu wa kuwa na Ulaya iliyo huru, kuimarisha urafiki na Ufaransa na kwamba ushirikiano na Marekani ni muhimu kwa sera ya kigeni ya serikali ijayo. Mwanasiasa huyo wa SPD ameahidi kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu na Marekani ulioanza tangu baada ya vita vya pili vya dunia.

Kansela huyo mtarajiwa, amesema vyama hivyo vitatu vimeungana kwa nia njema ya kuifanya Ujerumani iwe bora zaidi. Miongoni mwa mambo mengine mengi, Scholz ameahidi serikali ijayo itaongeza kima cha chini cha mshahara, pamoja na kuweka malengo makubwa zaidi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Vyanzo: (ap, afp, dpa, rtre)