1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani: SPD, Kijani na FDP kuanza mbio za kuunda serikali

Daniel Gakuba
15 Oktoba 2021

Olaf Scholz, mgombea wa ukansela wa Ujerumani wa SPD amepiga hatua katika safari ya kumrithi Angela Merkel, baada ya chama chake kupata makubaliano ya msingi na vyama vingine viwili, ya kuunda serikali ya muungano.

https://p.dw.com/p/41k0n
Pressekonferenz nach Ampel-Sondierungsgesprächen
(Kutoka kushoto) Robert Habeck, Annalena Baerbock (Viongozi wenza wa Kijani), Olaf Scholz (SPD) na Christian Lindner (FDP).Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Vyama hivyo vitatu vimekuwa katika mazungumzo tangu chama cha SPD cha sera za mrengo wa wastani wa kushoto,  kilipoongoza katika uchaguzi mkuu wa mwezi uliopita. Kambi ya vyama vya kihafidhina (CDU/CSU) ya kansela anayeondoka, Angela Merkel ilikuja katika nafasi ya pili, na nafasi yake ya kushirikishwa katika serikali ijayo inazidi kufifia.

Soma zaidi:  FDP, Kijani wakutana kwa mazungumzo ya serikali ya mseto Ujerumani

Akizungumza mchana wa leo, Scholz ambaye kwa sasa ni waziri wa fedha amesema mazungumzo yamekuwa marefu, lakini sasa kuna ishara kuwa vyama vyao vitatu, SPD, Kijani na FDP vinaweza kujadiliana juu ya namna ya kuunda serikali ya pamoja.

''Tumeafikiana kimaandishi, juu ya kuanza mazungumzo ya awali yatakayoweka msingi kwa vyama kufanya maamuzi yao. Kwa mtazamo wa yale ninayoyataka, hiyo ni habari njema, '' amesema Scholz na na kuongeza kuwa ni hatua inayoonyesha kuwa Ujerumani inaweza kuwa na ''serikali itakayoleta maendeleo yanayohitajika katika sekta nyingi za kijamii na kiuchumi, sambamba na malengo yetu kama nchi ya Ulaya.''

Deutschland Sondierungsgespräche l Ampel-Koalition l Olaf Scholz
Olaf Scholz, njia yake kuelekea ukansela inazidi kunyookaPicha: Christof Stache/AFP/Getty Images

Safari ya pamoja katika muongo wa kuanza upya

Mwenyekiti mwenza wa chama cha Kijani Annalena Baerbock ameafikiana na kauli hiyo ya Scholz, akisema muafaka uliopatikana unadhihirisha utashi wa vyama vinavyohusika kuufanya muongo ujao kuwa wa kuanza upya.

Soma zaidi: Armin Laschet hatimae ampongeza Scholz kwa ushindi

Pamoja na makubaliano hayo, chama cha Kijani na FDP vitalazimika kupunguza pengo la kimtazamo, lakini viongozi wa vyote viwili wamesema watapata maridhiano ili kuweza kuhudumu pamoja katika serikali kuu ya shirikisho.

Ingawa kiongozi wa CDU Armin Laschet ameshikilia kuwa bado anayo matumaini ya kushirikiana na vyama vingine kuunda serikali, habari za mchana wa leo ni pigo kubwa kwa matumaini hayo, na kitisho kwa nyadhifa nyingine alizo nazo.

Deutschland Berlin | Ampel-Koalition | Symbolbild
Rangi za vyama vya SPD (nyekundu), FDP (njano) na cha walinzi wa mazingira (kijani) zinafanya muungano wa vyama hivyo ujulikane kama wa 'Taa za barabarani'.Picha: Klaus-Dieter Esser/agrarmotive/picture alliance

Umma wavutiwa na mseto wa 'Taa za barabarani'

Serikali ya muungano ya SPD, Kijani na FDP maarufu kama 'Taa za barabarani' kutokana na rangi za vyama hivyo, yaani nyekundu, njano na kijani, imepata uungwaji mkono wa umma wa Ujerumani, huku uchunguzi wa maoni wa hivi karibu ukionyesha kuwa asilimia 62 ya Wajerumani wanataka serikali ya mseto ya vyama hivyo.

Soma zaidi: Ujerumani kuwa na serikali nyengine ya mseto

Umaarufu wa Olaf Scholz ni mkubwa hata zaidi ya hapo, ambapo watatu kati ya Wajerumani wanne wanasema itakuwa vyema akiwa kansela anayefuata.

Kubadili mrengo wa uongozi wa Ujerumani kuegemea sera za kushoto ambazo ni za kijamii zaidi kunatokea wakati nchi hiyo yenye uchumi imara zaidi barani Ulaya, ikikabiliwa na changamoto kubwa katika kuuweka sawa uchumi wake ulioathiriwa na janga la virusi vya corona.

rtre, afpe