1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimae Armin Laschet ampongeza Scholz

Saumu Mwasimba
30 Septemba 2021

Juhudi za kutafuta maelewano ya kuunda serikali zaendelea wakati miito ikitolewa kuwataka wanasiasa wajitahidi kutoa msimamo katikati ya Oktoba

https://p.dw.com/p/414lN
Nach der Bundestagswahl I Armin Laschet I CDU
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Juhudi za kutafuta maelewano ya kuunda serikali nchini Ujerumani zinaendelea na kansela Angela Merkel na mgombea aliyewania kumrithi kutoka kambi yake ya wahafidhina, Armin Laschet jana wamempongeza mgombea wa SPD Olaf Scholz aliyeshinda uchaguzi huo wa Jumapili.

Msemaji wa Kansela Angela Merkel ameeleza kwamba Kansela amempongeza Olaf Scholz kwa mafanikio aliyoyapata kwenye uchaguzi, wakati chama cha Christian Democratic CDU nacho kikisema hata mgombea wake Armin Laschet ametoa pongezi zake kwa mgombea wa Ukansela wa Social Democratic SPD, Olaf Scholz jana Jumatano. Laschet alikuwa akikosolewa sana kwa kushindwa kumpongeza mapema mpinzani wake huyo aliyeshinda uchaguzi wa Jumapili.

Deutschland | Live-Talk zur Energie- und Klimapolitik in Bderlin | Kanzlerkandidaten
Picha: Kay Nietfeld/dpa/picture alliance

Matokeo ya uchaguzi yameitumbukiza kambi ya wahafidhina kwenye mgogoro ambapo baadhi ya vigogo wa juu wameonesha kujiweka kando na Armin Laschet kiongozi wa CDU kusisitiza muda wote kwamba atajaribu kuunda serikali mpya ya mseto licha ya kushika nafasi ya pili kwenye uchaguzi wa Jumapili. Kansela Merkel ambaye anaondoka baada ya miaka 16 madarakani alikuwa kimya kipindi chote hiki lakini sasa ameuvunja ukimya huo kupitia taarifa hiyo iliyotolewa inayoonesha kwamba alimpongeza bwana Scholz toka Jumatatu.

Hivi sasa Scholz ambaye ni waziri wa fedha katika serikali ya mseto ya Kansela Merkel anatafuta namna ya kufikia makubaliano na chama cha Kijani kilichopata asilimia 14.8 ya kura pamoja na Free Democratic FDP kilichopata asilimia 11.5 ya kuunda serikali mpya alau kufikia Krismasi na anasema amekabidhiwa mamlaka na wapiga kura kuunda serikali ikiwezekana.

Hii leo alhamisi naibu kiongozi wa chama cha CDU ambaye ni waziri wa afya Jahn Spahn akizungumza na kituo cha redio cha taifa cha DeutschlandFunk-amesema vyama vya kisiasa vinapaswa kufikia mwafaka kufikia katikati ya mwezi Oktoba kuhusu nani watakaoshiriki kwenye mazungumzo rasmi ya kuunda serikali ya mseto,ili kila mmoja afahamu nchi inaelekea wapi.

Jumatano chama cha kijani cha wanamazingira walisema kwamba duru yao ya mwanzo ya mazungumzo ya ufafanuzi na Waliberali FDP ilikwenda vizuri ingawa ulijitokeza mvutano kuhusu ni chama gani kikubwa kati ya SPD na CDU wanachotaka kuingia nacho kwenye serikali mpya.

Deutschland | Nach der Bundestagswahl - Die Grünen
Picha: Andreas Gebert/AP Photo/picture alliance

Ikumbukwe kwamba The Greens au wanamazingira na FDP ndio wenye usemi wa nani ataunda pamoja nao serikali kati ya Scholz na Lachet. Chama cha Kijani kinapendelea kuwa kwenye serikali pamoja na FDP na SPD lakini Waliberali, FDP wanapendelea kuwa na serikali ya mseto pamoja na kambi ya CDU/CSU na Kijani.

Naibu kiongozi wa CDU Spahn kwa upande mwingine amesema huu sio wakati wa kujadili ikiwa Laschet abakie au aondoke kwenye uongozi wa chama akisema kwamba chama kimekubaliana Armin Laschet anapaswa kuongoza pamoja na kiongozi wa Bavaria Markus Soeder, mazungumzo ya mwanzo ya ufafanuzi kuhusu uundaji serikali ya mseto.