1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika watolewa mwito wa kuharakisha mikakati ya kupata madawa yanayofubaza virusi vya HIV

Epiphania Buzizi8 Juni 2005

Wajumbe wa mkutano wa kimataifa unaofanyika nchini Afrika ya Kusini, unaojadili mbinu za kupambana na ugonjwa wa UKIMWI barani Afrika wameeleza umuhimu wa ushirika wa serikali na sekta binafsi katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

https://p.dw.com/p/CHgd
Madawa ya kufubaza UKIMWI
Madawa ya kufubaza UKIMWIPicha: AP

Mkutano huo umewahimiza viongozi wa bara la Afrika kufanya hima na kuongeza juhudi za kutafuta madawa ya wananchi wake wanaokabiliwa na janga hilo kabla wajaugua na kufikia taabani.

Akizungumza na katika mkutano huo,mtaalam wa sayansi kutoka Botswana Ernest Darkoh, ambaye alifanikiwa katika mpango wa kutoa madawa kwa wagonjwa wa UKIMWI nchini humo, amesema ni jambo linalowezekana kwa mataifa ya Kiafrika kutafuta madawa ya kuwasaidia wagonjwa wa UKIMWI kwa kutumia raslimali iliyopo.

Mtaalam huyo ameeleza kuwa juhudi za pamoja zinahitajika katika kufikia mafanikio ya kuwapatia madawa mamilioni ya wagonjwa wa UKIMWI barani Afrika,na kwamba jambo hili linawezekana ikiwa kutakuwepo na ushirikiano kati ya serikali za mataifa na na sekta binafsi.

Wakati huo huo ,Erinest Darkoh amebainisha kuwa ni muhimu kwa watu kupima damu mapema na kujua hali zao kiafya,na hivyo kufanikisha kampeni ya kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo hatari.

Botswana,nchi ambayo ina idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya HIV, asilimia 40 ya watu wazima wakiwa na virusi hivyo, ilianzisha mpango wa kutoa madawa ya kupunguza makali ya magonjwa yanayowashambulia wenye virusi hivyo tangu mwaka 2002.

Kwa sasa nchi hiyo yenye jumla ya wakaazi milioni moja na nusu, inatoa dawa kwa watu elfu arubaini wenye virusi vya HIV.

Ernest Darkoh, mtaalam kutoka Botswana ,amesema mataifa mengine barani Afrika, yanaweza kuiga uzoefu wa nchi hiyo katika kukabiliana na ongezeko la watu wanaoambulikzwa virusi vya HIV,kwa kuanzisha mpango wa kupima damu kila mgonjwa anayekwenda kupata matibabu hospitalini.

Amesema hatua hiyo itasaidia kujua idadi ya wananchi walioambukizwa virusi hivyo, na kuwezesha serikali zao kuchukua mikakati ya kutafuta madawa ya kuwahudumia kabla hali zao hazijawa mbaya zaidi.

Nchi ya Afrika ya Kusini, jirani na Botswana, na ambayo ina watu wengi wenye virusi vya HIV wanaokadiriwa kufikia milioni 5, haijaonyesha juhudi kubwa katika kulishughulikia suala la kutoa madawa kwa raia wake wenye virusi hivyo.

Na wakati mkutano wa kimataifa unaojadili sera za kupata madawa kwa wagonjwa wa UKIMWI ukiendelea nchini humo, makundi ya wanawake waliopata virusi vya HIV, wameitolea mwito serikali yao kufanya hima na kuwasaidia raia wake ambao wanazidi kuangamia siku hadi siku kutokana na janga hilo.

Mwanamke wa kwanza nchini Afrika ya Kusini kutangaza hadharani kwamba aliambukizwa virusi vya HIV, Bi. Prudance Mabele, ametoa changamoto kwa serikali yake kuingilia kati na kufanya chochote kuwasaidia wagonjwa ambao wanahangaika kupata matibabu nchini humo.

Ameeleza kuwa wengi wa wagonjwa hao, wanatembea umbali wa kilomita 15 kwenda kupata huduma za matibabu.Kuna hospitali ambazo watu wanalazimika kulipa kwanza kabla ya kutibiwa.

Bi. Mabele amesema wakati umewadia kwa waziri wa afya nchini Afrika ya Kusini kujua hali ngumu inayowakabili watu wenye virusi vya HIV. Anasisitiza kuwa,serikali haina budi kujua matatizo yanayowakumba wananchi.

Kulingana na msemaji wa watu wenye virusi vya HIV nchini Afrika ya Kusini,wagonjwa wengi walikufa kwa sababu walikosa matibabu. Baadhi yao hukosa matibabu na kufariki kwa sababu ya kutokuwa na kadi za hospitali.

Wengine hawapati matibabu kwa muda mrefu kwa sababu wanapaswa kuandikisha majina yao kwenye orodha ndefu na kusubiri. Wakati umewadia kwa serikali kulichunguza suala hili upya. Alisisitiza msemaji huyo wa watu wanaoishi na virusi vya HIV.

Kwa upande wake waziri wa afya wa Afrika ya Kusini Bibi Manto Tshabalala Msimang, amesema kuna mengi ya kufanya katika sekta ya afya nchini humo, na serikali inafanya kila linalowezekana kukabiliana na hali hiyo.

Mwenyekiti wa mkutano huo wa kimataifa unaojadili sera za kupata madawa kwa wagonjwa wa UKIMWI, Profesa Lynn Morris ,amesema miaka miwili iliyopita tangu nchini Afrika ya Kusini kufanyike mkutano mwingine wa kupambana na UKIMWI, tayari yamekwisha patikana maendeleo fulani katika kupambana na janga hilo.

Miongoni mwa juhudi hizo ni kwamba kwa siku hizi watu wanapenda kuzungumzia ugonjwa wa UKIMWI.

Mipango iko mbioni pia kuanzisha kampeni za kutoa madawa ya kusaidia watu wenye virusi vya HIV, na vile vile unaandaliwa mpango wa jaribio la chanjo ya madawa ya kurefusha muda wa uhai wa wagonjwa wa UKIMWI.