1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika na Ulaya wakutana Luanda Angola

Amina Abubakar ap, reuters
24 Novemba 2025

Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika wanakutana Angola kwa mkutano wa siku mbili, unaolenga kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kiusalama, ambao utakuwa pia jukwaa la mazungumzo ya dharura kuhusu Ukraine.

https://p.dw.com/p/545eL
Angola Luanda 2025 | Mkutano wa EU-AU
Mazungumzo ya Ulaya na mataifa ya Afrika yatashughulikia masuala ya biashara, uhamiaji, amani, usalama, na malighafi muhimu Picha: Ndomba Borralho/DW

Emmanuel Macron wa Ufaransa, Friedrich Merz wa Ujerumani na William Ruto wa Kenya ni miongoni mwa viongozi kadhaa wa Umoja wa Ulaya na Afrika wanaotarajiwa kufika Luanda, Angola huku kukiwa na mvutano kati ya Marekani na Ulaya kuhusu mpango wa Washington wa kumaliza mgogoro wa Ukraine.

Mazungumzo na mataifa ya Afrika yatashughulikia masuala ya biashara, uhamiaji, amani, usalama, na malighafi muhimu, kabla tamko la pamoja kutolewa siku ya Jumanne (24.11.2025).

Ulaya inachangia vikosi vya kijeshi katika bara hilo kusaidia juhudi za kupambana na ugaidi, kuimarisha uthabiti na kuzuwia migogoro katika mataifa kama Libya, Mali, Somalia na Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Angola 2025 | Emmanuel Macron na Friedrich Merz
Emmanuel Macron wa Ufaransa na Friedrich Merz wa Ujerumani nwanashiriki mkutano huo wa Ulaya na Afrika nchini AngolaPicha: Yves Herman/REUTERS

Pande zote mbili Ulaya na Afrika zinatarajia kuongeza ushirikiano wao zaidi katika sehemu nyengine ikiwa ni miaka 25 tangu mkutano huo kwa mara ya kwanza kufanyika mjini Cairo Misri mwaka 2000.

Ulaya ni mshirika muhimu wa kibiashara  barani Afrika, huku mataifa ya Afrika kwa Ujumla, yakiwa mchangiaji muhimu wa nne  wa Ulaya hii ikiwa ni kulingana na data za Umoja huo. Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya imesema mwaka 2023 pekee bara hilo liliwekeza dola bilioni 275 barani Afrika.

Mkutano huu wa saba kati ya EU na AU huko Luanda, unafanyika siku moja baada ya kumalizika mkutano wa kilele wa kundi la mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi duniani G20, uliofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika, nchini Afrika Kusini.