1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vigogo vya ligi ya mabingwa vyaendelea kutesa

Sekione Kitojo20 Oktoba 2010

Timu za ligi kuu ya Uingereza Arsenal na Chelsea , Bayern Munich na Real Madrid zaendelea kupata ushindi.

https://p.dw.com/p/PiNj
Mchezaji wa Arsenal London Carlos Vela akishangilia bao.Picha: AP

Timu  za  ligi  kuu  ya  Uingereza  Arsenal  na  Chelsea pamoja  na  Bayern  Munich  ya  Ujerumani   na  Real Madrid  ya  Hispania  zimeendelea  jana  usiku  kuelekea katika   kukata  tikiti  ya  kushiriki  katika  awamu  ya michezo  ya  mtoano  katika   ligi  ya  mabingwa  barani Ulaya, Champions League  wakati  kila  moja  ilifanikiwa kushinda  kwa  mara  ya  tatu  katika  michezo  mitatu  hadi sasa  ya  ligi  hiyo  ya  mabingwa.

Mjini  Munich, CFR  Cluj  wageni  wa  Bayern  Munich kutoka  Romania  walipachika   wavuni  mabao  manne  kati ya  matano  usiku  wa  jana , lakini  mawili  kati  ya  hayo yalitumbukia   katika  nyavu  zao  wakati  wenyeji  wao Bayern  Munich  wakishinda  pambano  hilo  kwa  mabao 3-2, wakati  huo  huo  Real  Madrid  iliweka  msingi  wa ushindi  wa  mabao  2-0  dhidi  ya  AC Milan  katika  kipindi cha  kwanza  cha  pambano  lao.

Arsenal  london  ilionyesha  kuwa  ni  mzigo  mzito  kwa Shakhtar  Donetsk, na  kuirarua  timu  hiyo  kwa  mabao  5-1, wakati  Chelsea  London  nayo  ilishinda  kwa  mabao  2-0  dhidi  ya  Spartak  Moscow.

Bundesliga Spieltag 33 Bayern München Vfl Bochum Louis van Gaal Thomas Mueller Flash-Galerie
Kocha wa Bayern Munich Louis van Gaal akimpongeza mchezaji wake Thomas Müller.Picha: AP

Mjini  Munich  mashabiki  64,000  walishuhudia   mlinzi raia  wa  Ureno  Cadu  akiwashangaza  kwa  kupachika bao   dhidi  ya  timu  hiyo  ya  kocha  Luis  van Gaaal  , katika  dakika  ya  28, lakini  dakika  nne  baadaye  aligeuka kutoka  kuwa  shujaa  na  kuwa  wa  kulaumiwa  baada  ya kuutumbukiwa  mpira  uliopigwa  na  Toni  Kroos  katika nyavu  zake.

Bayern  ilichukua  uongozi  wa  mchezo  huo  kwa  bao  la dakika  ya  37  wakati    mpira  wa  kona  ulipomgonga Cristian  Panin  gotini  na  kuingia  wavuni. Mario  Gomez aliihakikishia  Bayern  Munich  ushindi  wa  mchezo  huo katika  dakika  ya  77  wakati  Cadu  alipojaribu  kuuondoa mpira   huo, lakini  uligonga  tena  Gomez  na  kujaa wavuni.

Juan  Culio  aliufumania  mlango  wa  Bayern  zikiwa zimesalia  dakika  nne  mpira  kumalizika , lakini  ilikuwa bahati  mvaya  tena  kwa  wageni  hao  kutoka  Romania kuweza  kurejesha  mabao  yote.

Binafsi  Mario  Gomez  amekiri  kuwa  goli  lake  lilikuwa zaidi  kama  goli  la  kujifunga  wenyewe  kuliko  juhudi zake. Tunahitaji  kuwashuruku  Cluj  kwa  mabao  yote matatu. Lakini  hii  ni  soka , wakati  mwingine  mambo yanakwenda  upande  wako, amesema  Gomez.

Mmeona  jinsi  ilivyo  vigumu  kucheza  na  timu  ambayo inacheza  kwa  kujihami  mno, lakini  nimefarijika   kuwa nafunga  magoli  na  kwamba   napata  nafasi   tena  ya kucheza.

Kocha  wa  Bayern  Munich  Louis van Gaal  amesema kuwa  timu  yake  ilistahili  kupata  bahati  iliyopata. Hatuna bahati  msimu  huu, kwa  hiyo  bahati  kidogo  katika mchezo  ni  jambo  la  kufurahisha. Ni  vigumu  ikiwa  timu pinzani  inacheza   na  watu  kumi   katika  ulinzi.Nafikiri wachezaji  wetu  wa  kati  wamefanya  kazi  nzuri. Waliweza kuufanya  mpira  uzunguke  huku  na  huko  na  kuwaweka wapinzani  wetu  katika  mbinyo.

Katika  mchezo  mwingine  wa  kundi  E Basel iliwashangaza  AS Roma  kwa  kuichapa  mabao  3-1. Real Madrid  ilifanikiwa  kupachika  mabao  2  kupitia  Cristiano Ronaldo  na  Mesut Özil  katika  kipindi  cha  dakika  moja katika  mchezo  wao  wa  kundi  G  dhidi  ya  AC Milan.

Ronaldo  amesema  kuwa  walianza  mchezo  huo wakijihisi  kuwa  na  uwezo, tulifahamu  kuwa  tunacheza na  timu  yenye  uzoefu na  tulihitaji  kuwashambulia, na kama  tutafanya  hivyo  hawataweza  kuhimili. Kocha  Jose Mourinho, aliwasifu  wachezaji  wake  kwa  kusema ninafuraha  sana   kwa  matokeo  haya  na  nina  furaha kutokana  na  jinsi  timu  ilivyocheza  na  kuonyesha juhudi. Nafikiri  timu  hii  ilicheza mchezo  kamili.

Ajax Amsterdam  iliishinda  Auxerre  kwa  mabao  2-1 wakati  Sporting  Braga  walipata  points  zao  za  mwanzo katika  kinyang'anyiro  hiki   kwa  kuizamisha  Partizan Belgrade  kwa  mabao  2-0  nyumbani  Ureno.

Katika  mchezo   uliochezwa  mwanzo  Chelsea  ilichukua usukani  wa  kundi  F  baada  ya  kuishinda  Spartak Moscow  kwa  mabao 2-0. Nayo Olympique  Marseille ilipata  ushindi  wa  bao  1-0  dhidi  ya  Zilina  ya  Slovakia.