Utafiti wa afya barani Afrika wakabiliwa na ukosefu wa fedha | Masuala ya Jamii | DW | 15.12.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Utafiti wa afya barani Afrika wakabiliwa na ukosefu wa fedha

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa baada ya uchunguzi katika sekta ya afya barani Afrika, utafiti barani humo na uvumbuzi unakwamishwa na uhaba wa fedha

default

Maabara za Afrika zinakabiliwa na ukosefu wa fedha

Maabara za afya Afrika zina shughuli nyingi za uvumbuzi wa kukabiliana na magonjwa yanayolizonga bara hilo lakini mikakati hiyo inakwama kutokana na ukosefu wa fedha.Maabara za afya Afrika zina shuhguli nyingi za uvumbuzi wa kukabiliana na magonjwa yanayolizonga bara hilo lakini mikakati hiyo inakwama kutokana na ukosefu wa fedha.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la sayansi, umetambua miradi 25 iliyokwama licha ya kupangwa kwa ufasaha. Ken Simiyu aliyeandika ripoti hiyo kwa ushirikiano na taasisi ya utafiti wa afya ya McLaughlin-Rotman, nchini Canada, anasema jitihada za wawekezaji na wavumbuzi zinazotumia teknolojia ya kisasa kuboresha afya, zinavurugwa na miundo mbinu mibovu barani Afrika.

Bw Simiyu anasema kwamba Waafrika wengi wana talanta licha ya vikwazo hivyo. Kwa mfano uvumbuzi uliofanywa nchini Ghana na kukagunduliwa mbinu ya kukabiliana na ugonjwa unaosababishwa na vijidudu vya Schistosoma vinavyowaathiri asilimia 50 ya watu hasa wanaoishi kusini mwa jangwa la Sahara.

Nchini Uganda, kifaa cha kutupia takataka kutoka hospitalini kiliundwa ili kupunguza tatizo la kuzagaa kwa uchafu katika hospitali za mashinani, lakini kifaa hicho hakijafaulu kuingia katika masoko. Dawa mbadala ya kutibu Malaria nchini Ghana iitwayo, Nibima haijaangaziwa ili isaidie katika vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria.

Bw Simiyu anasema tatizo sio la ukosefu wa fedha tu, bali pia ni suala la kuingiza siasa zinazovuruga mikakati ya kuendeleza uvumbuzi.

Mataifa mengi barani Afrika, hutenga kiasi cha asilimia 0.2 hadi asilimia 0.3 ya pato la ndani, katika kufadhili utafiti wa afya na maendeleo na ni upungufu wa kama mara kumi ya viwango vya mataifa yaliyoendelea.

Wanasayansi wanaohusika katika uvumbuzi wamekuwa pia wakikosa washirika na utaalamu wa kuwezesha bidhaa kusajiliwa kisheria na hatimaye kupata soko.

Taasisi ya utafiti wa afya nchini Kenya, KEMRI kwa mfano ilijenga kiwanda cha kutengeneza vifaa vya kupima na uwepo wa virusi vya HIV na ugonjwa wa Hepatitis lakini kiwanda hicho hadi wa leo hakifanyi kazi kwa sababu ya kubadilishwa kwa sera ya serikali ambayo ilifaa kukinunua.

Utafiti huo pia unatambua mifano ya jitihada zilizofaulu kama ya kampuni ya nguo ya A to Z nchini Tanzania ambayo ilifaulu kuzuia vikwazo vya utendaji kazi na sasa ni kati ya makampuni makubwa yanayotengeneza vyandarua vya kuzuia mbu.

Katika kitambulisho cha utafiti huo, Profesa Calistous Juma wa chuo kikuu cha Harvard, alielezea wasiwasi wake kuhusu tatizo la kupata madawa ambalo limekuwa likijadiliwa katika mazungumzo ya sera ya afya kwa miaka mingi, lenye dhana potovu kwamba bara la Afrika litaendelea kutegemea uagizaji wa bidhaa kutoka nje.

Mkurugenzi wa taasisi ya McLaughlin-Rotman iliyochapisha utafiti huo, Peter Singer, alisema nyaraka zilizokusanywa katika utafiti huo, zinaonyesha taswira tofauti na kwamba kati ya uvumbuzi 25, miradi 16 inafaa kufadhiliwa, hasa inayohusu madawa mbadala ya kienyeji.

Alisema kwamba kinachohitajika ni taasisi ya ubunifu na sera madhubuti itakayopunguza hatari na kuendeleza juhudi za mashinani ili kuhakikisha kuna manufaa zaidi katika uvumbuzi wa utafiti katika sekta ya afya.

Bw Singer alikariri kwamba watu wengi watafariki ikiwa Afrika itaendelea kuwasubiri wanasayansi kutoka nje kuvumbua na kutafuta masoko ya bidhaa za afya zinazohitajika barani humo.

Mwandishi: Peter Moss /AFP

Mhariri: Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com