Upinzani wataka marufuku ya ndege kutoruka katika anga ya Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.09.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Upinzani wataka marufuku ya ndege kutoruka katika anga ya Syria

Upinzani nchini Syria unataka nchi hiyo iwekewe marufuku ya ndege kutoruka katika anga yake kwa lengo la kuwalinda raia dhidi ya ukandamizaji unaofanywa na serikali.

default

Rais wa Syria, Bashar al Assad

Muungano unaoyawakilisha makundi 40 ya upinzani nchini Syria umeitaka jumuiya ya kimataifa iunge mkono marufuku ya ndege kutoruka katika anga ya nchi hiyo kuwalinda raia dhidi ya ukandamizaji wa umwagaji damu unaofanywa na utawala wa rais Bashar al Assad. Muungano huo unaojiita "Kamisheni ya Mapinduzi ya Syria" unapinga kile inachosema ni uhalifu dhidi ya ubinaadamu katika hatua ya serikali kuwashambulia wanaharakati wanaopigania demokrasia nchini humo.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Washington, Marekani hapo jana, muungano huo hata hivyo ulisema hautaki harakati ya kijeshi ya nchi za kigeni katika ardhi ya Syria. Badala yake unataka jumuiya ya kimataifa iingilie kati kwa kutuma tume ya kulinda amani, ukisema serikali imewatuma wanajeshi kwa lengo la kufanikisha mfumo wa ukandamizaji wa maonevu, mateso na maangamizi makubwa.

Kundi moja katika muungano huo, limetaka Syria iwekewe vikwazo vya silaha vitakavyoyalazimisha mataifa, hasa yale yanayopaka na nchi za Mashariki ya Kati, kuchunguza mizigo inayoingia na kutoka nchini humo. Kundi lengine limetaka mali za Syria zizuiliwe.

Taarifa iliyosainiwa na makundi hayo itawasilishwa kwa ofisi ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, baraza la usalama la umoja huo na kwa rais wa Marekani, Barack Obama.

Nchi za Ulaya zawasilisha azimio

Awali nchi za Ulaya zilitangaza azimio jipya kuhusu Syria linalohimiza kitisho cha vikwazo badala ya vikwazo vya haraka. Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Ureno zilisambaza rasimu ya azimio hilo kuilaani Syria linalojumuisha kitisho cha vikwazo iwapo serikali ya rais Assad haitakomesha ukandamizaji dhidi ya raia. Iwapo litapitishwa, baraza la usalama kupitia azimio hilo litaelezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali nchini Syria na kutaka machafuko yakomeshwe mara moja.

Mwezi uliopita Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Ureno ziliwasilisha pendekezo la azimio lililotaka vikwazo dhidi ya rais Assad, jamaa wa familia yake wenye ushawishi mkubwa na wapambe wake wa karibu. Kundi la nchi zenye uchumi unaoinukia, zikiwemo Urusi, China pamoja na Brazil, India na Afrika Kusini, zilipinga azimio hilo la awali. Wanadiplomasia wa mataifa ya magharibi wanasema azimio hilo jipya litakubalika zaidi na nchi hizo.

Hali ni ngumu nchini Syria

Nchini Syria kwenyewe hali ya kimaisha imeendelea kuwa ngumu, huku uchumi ukiathirika kutokana na vikwazo. Björn Luley, mkufunzi katika taasisi ya Goethe mjini Damascus ambayo ilifungwa mwezi Aprili mwaka huu, anasema, "Kwamba hatimaye hali ngumu ya kiuchumi kutokana na vikwazo hivi ndiyo itakayotoa maamuzi ya mwisho. Na viongozi watashinikizwa kwa haraka zaidi kufanya mageuzi ya kisiasa nchini Syria kupitia vikwazo hivi kuliko maandamano."

Wakati huo huo, raia tisa waliuwawa jana wakati vikosi vya usalama vilipowavamia wapinzani wa serikali. Watu sita waliuwawa katika mji wa Homs katikati ya nchi huku wengine wawili wakiuliwa katika mji wa kaskazini magharibi wa Idlib. Shirika la haki za binaadamu nchini Syria limesema mtu mmoja aliuwawa katika mkoa wa kusini wa Daraa, kulikoanzia maandamano mwezi Machi mwaka huu.

Shirika hilo limesema silaha nzito zilitumika dhidi ya raia, siku moja tu baada ya wanajeshi wanne kupigwa risasi na kuuwawa wakati walipojaribu kulikimbia jeshi.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE

Mhariri: Hamidou Oummilkheir

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com