Umoja wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo vya silaha? | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.07.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Umoja wa Ulaya kuiwekea Urusi vikwazo vya silaha?

Huenda Umoja wa Ulaya ukazingatia vikwazo vya silaha dhidi ya Urusi, huku Australia ikitoa wito wa eneo ilipoangukia ndege ya Malaysia mashariki mwa Ukraine kulindwa na kikosi cha kimataifa.

Mwakilishi wa kundi linalopigania kujitenga na Ukraine (kushoto) akipeana mkono na mwakilishi wa Baraza la Usalama la Malaysia baada ya kukabidhi kisanduku cheusi cha ndege ya Malaysia aina ya MH17.

Mwakilishi wa kundi linalopigania kujitenga na Ukraine (kushoto) akipeana mkono na mwakilishi wa Baraza la Usalama la Malaysia baada ya kukabidhi kisanduku cheusi cha ndege ya Malaysia aina ya MH17.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, Philip Hammond, amesema kuwa msiba huu wa ndege aina ya MH17 ya Malaysia umesababishwa na msaada wa Urusi kwa waasi wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine na kwamba lazima mawaziri wa nje wanaokutana leo mjini Brussels lazima walijadili hilo.

Kwa mujibu wa Hammond, licha ya kuwa tayari mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya uliofanyika Jumatano ulipendekeza kuongezwa kwa vikwazo dhidi ya viongozi wa Urusi na Ukraine, lakini kuangushwa kwa ndege hiyo sasa kumeifanya hali ibadilike zaidi.

"Dunia imebadilika pakubwa tangu ajali hii na sasa nasi tunapaswa kusogea mbele zaidi. Vikwazo vya silaha ni moja ya mambo tutakayopaswa kuyazingatia. Umoja wa Ulaya unapaswa kutuma ujumbe wa wazi kwa Urusi." Alisema Hammod wakati akiwasili mjini Brussels hivi leo.

Msimamo kama huu umeungwa mkono na mawaziri wengine wa nje, kama vile Linas Linkevicius wa Lithuania ambaye amehoji kwamba waasi wa mashariki mwa Ukraine wanapaswa kuchukuliwa kama magaidi, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden akisema ni jambo gumu sana kutetea suala la kuipa silaha Urusi kwa sasa.

Australia yataka kikosi cha kimataifa

Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott.

Waziri Mkuu wa Australia, Tony Abbott.

Kwengineko duniani, sala za kuwakumbuka na kuwaombea watu waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo mbaya kabisa tangu ile ya kupotea kwa ndege nyengine ya Malaysia, MH370, ilipopotea mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka huu ikiwa na watu 239.

Akizungumzwa kwenye ibada hiyo hivi leo, Waziri Mkuu wa Australia Tony Abbott, ambaye nchi yake imepoteza raia 27 kati ya watu 298 waliokuwamo kwenye MH17, amesema hivi nchi "zilizotendewa makosa" kwenye mkasa huu, lazima zipewe dhamana ya kulilinda eneo la tukio, akizitaja Malaysia, Uholanzi na nchi yake kuwa na haki hiyo.

"Kikosi cha polisi ya mataifa mchanganyiko au jeshi la aina hiyo si kitu ambacho kinaweza kuitishwa kwa kipindi cha masaa machache. Lakini kwa hakika panapaswa kuwepo usalama kwenye eneo hilo na nafikiria ulinzi wa eneo hilo utatolewa kwa uhakika zaidi na nchi ambazo zimekosewa. Na hilo naamini litakuwa jambo jema kufanyika."

Mnamo mwisho wa wiki, viongozi wa Ufaransa, Uingereza na Ujerumani waliionya Urusi kwamba itakabiliwa na vikwazo zaidi vya Umoja wa Ulaya ikiwa haikuwashinikiza waasi kuwaruhusu wachunguzi huru kufika eneo ilikoangukia ndege hiyo ya Malaysia.

Tangu kutolewa kwa kauli hiyo, tayari waasi wameshakabidhi kisanduku cheusi kwa mamlaka za Malaysia na zaidi ya miili 200 kwa wachunguzi. Treni iliyobeba miili hiyo inatazamiwa kuwasili nchini Uholanzi wakati wowote kutoka sasa, ambako nako itatambuliwa kabla ya kusafirishwa kwenye nchi zao kwa mazishi.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com