Ukraine na Uhusiano wa Ufaransa na Ujerumani | Magazetini | DW | 20.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Ukraine na Uhusiano wa Ufaransa na Ujerumani

Hali inayozidi kutokota nchini Ukraine na mkutano wa kilele kati ya Ujerumani na Ufaransa ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Maandamano yamepamba moto mjini Kiev

Maandamano yamepamba moto mjini Kiev

Tuanzie Ukraine ambako vuta nikuvute kati ya kambi ya serikali ya Rais Viktor Yanukovich na ile ya upande wa upinzani ingali inaendelea. Kwa mujibu wa habari za hivi punde watu kadhaa wameuwawa hii leo. Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linajiuliza Umoja wa Ulaya ufanye nini ?

"Haustahiki kufanya pupa, lakini wakati huo huo unabidi usimame kidete. Uamuzi wa kuzuwia mali ya ukoo wa Yanukovich na matajiri wa nchi hiyo pamoja na kuwafungia njia ya kuja kutembea katika maduka ya anasa ya nchi za Magharibi ni wa maana. Lakini hiyo isiangaliwe kuwa ni adhabu bali njia ya kuwashinikiza viongozi wa mjini Kiev waone umuhimu wa kuketi katika meza ya mazungumzo pamoja na wawakilishi wa upande wa upinzani. Umoja wa Ulaya unabidi uyaunge mkono Mazungumzo kama hayo kikamilifu.Hatimaye lakini, na hapa watu wasijihadae, la muhimu sio kuiona nchi hiyo ikielekea upande wa Magharibi. Au demokrasia timamu ikitawala. Bali, ikiwezekana, pengine maridhiano yapatikane. Kwa sababu Ukraine imegawika vibaya sana - hali ikizidi kuwa mbaya, hakuna yeyote atakayeibuka na ushindi. Hasara tu ndio itakayopatikana."

Gazeti la "Nordwest-Zeitung" la mjini Oldenburg linahisi pia mazungumzo ndio njia pekee ya kuufumbua mzozo wa Ukraine. Gazeti linaendelea kuandika:"Kuzidi makali kwa matumizi ya nguvu nchini Ukraine ni matokeo ya ung'ang'anizi wa kambi mbili zinazozozana. Kwa upande mmoja, kambi ya serikali inayotegemea msaada wa kisiasa na kiuchumi kutoka Urusi na kwa upande wa pili ,upande wa upinzani unaoelemea nchi za Magharibi unaohisi mustakbali wa nchi hiyo utategemea na kujiunga kwake na Umoja wa Ulaya. Kila upande unatoa masharti magumu kuweza kushiriki katika mazungumzo. Lakini ufumbuzi utapatikana tu kupitia meza ya mazungumzo. Tutaraji tu kwamba pande zinazohusika zitautambua ukweli huo kabla ya vita vya Kiev kuenea nchi nzima."

Uhusiano hauna Shida kati ya Ujerumani na Ufaransa

Merkel und Hollande in Paris

Rais Francois Hollande akiamkiana na kansela Angela Merkel alipowasili Paris kuhudhuria mkutano wa 16 wa mabaraza ya mawaziri wa nchi zao

Mkutano wa serikali ya Ujerumani na ile ya Ufaransa uliofanyika jana mjini Paris umechambuliwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani. Gazeti la "Dresdner-Neueste Nachrichten" linaandika:"Mkutano wa kilele kati ya Ujerumani na Ufaransa ni wa kuelezea dhamiri tu. Naiwe katika suala la kodi ya mapato katika shughuli za fedha, sera ya pamoja ya ulinzi au kupanuliwa miradi ya nishati mbadala - yote hayo ni maneno matupu tu, utekelezaji ni haba. Katika wakati ambapo mnamo siku chache tu zilizopita Francois Hollande na Barack Obama wamesherehekea kuchipuka upya enzi ya urafiki kati ya Ufaransa na Marekani, injini ya Ujerumani na Ufaransa ingali bado inajikokota. Cha kutia moyo pekee ni ule ukweli kwamba uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa kwa mtazamano wa kila siku ni madhubuti kuliko ile picha ya kulegalega inayojitokeza katika daraja ya uongozi."

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Mohammed Khelef