UKIMWI wapiga hodi kwa viongozi Barani Afrika! | Masuala ya Jamii | DW | 04.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

UKIMWI wapiga hodi kwa viongozi Barani Afrika!

UKIMWI yummkini ukawa unauwa maafisa wa serikali waliochaguliwa katika baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika kwa haraka sana kuliko vile nafasi zao zinavyoweza kuzibwa na hiyo kutowa tishio jipya kwa demokrasia katika eneo hilo.

Wasichana wadogo walioathirika na UKIMWI nchini Afrika Kusini.

Wasichana wadogo walioathirika na UKIMWI nchini Afrika Kusini.

Taasisi kwa ajili ya Demokrasia nchini Afrika Kusini IDASA imesema katika utafiti wa nyendo za vifo nchini Afrika Kusini Malawi,Namibia,Zambia,Tanzania na Senegal zinadokeza kwamba matatizo ya virusi vya HIV na UKIMWI yamepiga hodi kwa viongozi wa waliochaguliwa serikalini.

Kondwani Chirambo mkuu wa utawala na mpango juu ya UKIMWI katika taasisi ya IDASA amesema katika mkutano wa hivi karibuni mjini Cape Town kwamba utafiti wao umeonyesha kwamba kumekuwepo na ongezeko kubwa la idadi ya viongozi waliochaguliwa kufariki na mapema kutokana na UKIMWI.

Afrika Kusini imekuwa katika kampeni kubwa ya kupiga vita UKIMWI kwa kushajiisha matumizi ya mipira ya kondomu mfano katika jimbo la Hautei lenye kujumuisha miji ya Johannesburg na Pretoria ambapo hugawa bure mipira ya kondumu takriban milioni mbili au hata na zaidi kwa mwezi kwa wakaazi wake milioni kumi.

Kati ya mwaka 1994 na mwaka 2006 kumekuwepo na nafasi tupu 23 za ajira katika bunge la Afrika Kusini kutokana na kufariki kwa wabunge.

Wakati athari za janga hilo kwa maisha ya binaadamu na gharama za matibabu imeorodheshwa vyema utafiti wa IDASA umeonyesha kwamba virusi vya HIV na UKIMWI pia vinahusika katika mabadiliko ya madaraka ya kisiasa pamoja na kuupa mzigo mkubwa hazina ambapo inabidi kuandaliwe chaguzi mpya.

Eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara lina watu kama milioni 25 kati ya watu milioni 39 walioambukizwa virusi vya HIV na UKIMWI duniani kote tatizo ambalo linazidi kuwa zito kwa tabaka mbali mbali katika jamii.

Utafiti wa IDASA unatowa mwanga mpya juu ya tatizo la virusi vya HIV na UKIMWI wakati Afrika Kusini ikianza mkutano wake wa UKIMWI leo hii ambao hufanyika mwaka mara mbili.

Nchini Malawi utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kwamba jumla ya wabunge 42 wamefariki kati ya mwaka 1994 na mwaka 2006.Katika taarifa rasmi hapo mwaka 2000 spika wa bunge la taifa amesema miongoni mwa vifo hivyo 28 vimetokana na UKIMWI.

Katika nchi jirani ya Zambia katika kipindi cha miaka 20 kati ya mwaka 1964 wakati wa uhuru hadi mwaka 1984 wakati kesi ya kwanza ya UKIMWI iliporepotiwa ni chaguzi ndogo 14 kati ya 46 zilifanyika ikiwa kama ni matokeo ya vifo.Kati ya mwaka 1985 na mwaka 2003 zimefanyika chaguzi ndogo 102 na 29 miongoni mwa hizo zimetokana na maafisa kufariki wakiwa katika madaraka.

Ni vifo vichache vya viongozi barani Afrika hutajwa kuwa vimesababishwa na UKIMI jambo ambalo linaonyesha kujikita mno kwa unyanyapaa kunakoendelea kuandamana na gonjwa hilo barani kote Afrika.

 • Tarehe 04.06.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHkh
 • Tarehe 04.06.2007
 • Mwandishi Mohamed Dahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHkh

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com