1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawatuliza raia wake baada ya IS kurejea nchini

15 Novemba 2019

Serikali kuu ya Ujerumani inajaribu kuwatuliza wananchi kuwa usalama wao hautoingia hatarini kwa kurejea humu nchini wafuasi wa kundi la itikadi kali linalojiita Dola la Kiislam-IS kutoka Uturuki.

https://p.dw.com/p/3T646
Armin Schuster
Picha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Familia ya wanamgambo saba wa Kijerumani wanachama wa IS wamewasili Berlin jana baada ya wizara ya mambo ya ndani ya Uturuki kutangaza mapema wiki hii itaanza kuwarejesha wafuasi wote wa IS waliokamatwa.

Hakuna waranti uliotangazwa na Ujerumani dhidi ya familia moja ya wajerumani wenye asili ya Iraq, Kanan B, ikimaanisha wana  uhuru wa kurejea  majumbani mwao katika jimbo la kati la Lower Saxony, lakini watakuwa wakichunguzwa na polisi.

Kwa mujibu wa maafisa wa serikali ya Uturuki, Kanan B alijaribu kusafiri kwenda Syria pamoja na familia yake mwaka mmoja uliopita, lakini haijulikani kama alifika. Familia hiyo, wakiwemo, mtu na mkewe na watoto wao wawili wakubwa na watatu wadogo wamekuwa wakishikiliwa rumande tangu mwezi Machi uliopita katika mji wa Uturuki wa Izmir.

Maafisa wa serikali ya Ujerumani wanasema hawaamini kama familia ya Kanan B waliwahi kujiunga na magaidi wa itikadi kali wa IS, pengine walikuwa wafuasi wa itikadi kali ikimaanisha wote katika familia hiyo wamekuwa wakifuata muongozo asilia wa dini ya kiislam.

Raia wa Ujerumani watakaorejea "sio kitisho"

Ein irakischer Soldat
Bendera ya wanamgambo wa dola la kiislamu IS Picha: picture-lliance/AP Photo/K. Mohammed

Msemaji wa sera ya ndani katika chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU, Armin Schuster amesisitiza akisema kwamba raia wa Ujerumani watakaorejea "sio kitisho", ametahadharisha dhidi ya hisia za hofu na wasi wasi zinazoenezwa na vyombo vya habari.

"Hawajashiriki katika mapigano" amesema katika maahojiano na kituo cha matangazo cha Deutschland Radio. "Hawatotiwa jela" lakini watakuwa wakichunguzwa". "Ameongeza kusema kahia zitachunguzwa kwa kina na kwamba utaratibu kama huo ni wa kawaida kwa vikosi vya usalama nchini Ujerumani.

Armin Schuster amekanusha pia ripoti kwamba tangazo la Uturuki limepokelewa kwa mshangao mkubwa nchini Ujerumani na kwamba viongozi wa mjini Ankara hawakutoa maelezo mapema kuhusu kurejeshwa Ujerumani watu hao.

Kadhia ya Wajerumani wengine wawili watakaorejeshwa na Uturuki siku zinazokuja ni tete kidogo amesema Armin Schuster. Mabibi hao wawili tayari wanachunguzwa na polisi nchini Ujerumani na watabidi wakachukuliwe na polisi watakapowasili uwanja wa ndege, wahojiwe na pia kupekuliwa. Mwendesha mashitaka ndie atakaeamua baadae kama kuna ushahidi wa kutosha kuwakamata au la.

Vyama vya upinzani n chini Ujerumani vinakosoa kile wanachokitaja kuwa uzembe wa serikali kulishughulikia mapema suala hilo.

Chanzo dw.com