1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaonya kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi

Lilian Mtono
6 Oktoba 2019

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Horst Seehofer ameonya kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi zaidi ya lililoshuhudiwa barani Ulaya mnamo mwaka 2015.

https://p.dw.com/p/3QnD9
Die Lage der Flüchtlinge auf Lesbos
Picha: DW/D. Tosidis

Kwenye ziara hiyo Seehorfer Magazetini: Kuimarishwa kwa sheria ya waomba hifadhialiyeongozana na rais mpya wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, waziri huyo wa mambo ya ndani pia amesema Umoja wa Ulaya bado unatakiwa kuchukua hatua zaidi kuisaidia Uturuki, ili kuwazuia wakimbizi kujaribu kutumia njia hatari kuvuka na kuingia Ugiriki.

"Tunatakiwa kuwasaidia hata zaidi washirika wetu wa Ulaya kufanya doria kwenye mipaka ya nje ya Ulaya; tumewaacha peke yao kwa muda mrefu", Seehofer aliliambia gazeti la Bild am Sonntag la Ujerumani, akizingatia sio tu Ugiriki, lakini pia Uhispania na Italia. "kama hatutafanya hivyo, kwa mara nyingine tutashuhudia wimbi kubwa la wakimbizi kama la mwaka 2015 - na labda kubwa zaidi ya lile la miaka minne iliyopita."

Seehofer amesema Ulaya inatakiwa kujizuia na mzozo ambao haujajiandaa kuukabili, kama ilivyotokea mwaka 2015. Alifafanua kwamba anaungwa mkono kikamilifu na kansela Angela Merkel, ambaye huko nyuma walitofautiana wazi wazi kuhusu sera kuelekea wakimbizi.

Europa Migranten l weitere Flüchtlinge fliehen nach Griechenland
Wahamiaji na wakimbizi wakipanda meli kwenye bandari ya Mytilene, Lesbos.Picha: Getty Images/AFP/Stringer

Kwenye mahojiano tofauti na gazeti la Welt am Sonntag, Seehofer pia amesema Umoja wa Ulaya unatakiwa kufanya zaidi kuisaidia Uturuki kukabiliana na mamilioni ya wakimbizi walioingia nchini humo tangu kuanza kwa vita vya Syria mwaka 2011.

"Uturuki inafanya vizuri kuwakaribisha wakimbizi," amesema Seehofer. "lakini pia ni sehemu ya maslahi yetu, na ni lazima tujue kwamba hatutaweza kufanikiwa huko mbeleni kwa rasilimali za zamani."

Mwaka 2016, Umoja wa Ulaya ulikubaliana kuipatia Uturuki Euro bilioni 6, kuisaidia kutekeleza miradi yake inayohusiana na wakimbizi wa Syria. Hata hivyo, tangu wakati huo, Ankara imekuwa ikishambuliwa kwa kushindwa kusalia kwenye makubaliano ya kuwarejesha waomba hifadhi.

Deutschland Horst Seehofer in Erding
Waziri wa mambo ya ndani ya Ujerumani Horst Seehofer anataka kuchukuliwa hatua zaidi.Picha: picture-alliance/Sven Simon

Kwenye ziara hiyo ya siku mbili, Seehofer alizuru Uturuki na Ugiriki ambako alifanya mazungumzo na wawakilishi wa serikali, kwa matarajio ya kuingia makubaliano thabiti kuhusu wakimbizi na udhibiti wa mipaka.

Kusaka suluhu.

Seehofer, mapema alisema Ujerumani itachukua robo ya waomba hifadhi wote waliookolewa wakati wakijaribu kuvuka kuingia Ulaya kwa kutumia njia hatari ya bahari ya Mediterania.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa wa chama cha Ujerumani cha Christian Democrats, CDU na Freedom Democrats, FDP waliyapinga vikali mapendekezo hayo wakisema kwamba huenda yakavutia wakimbizi zaidi kuingia Ulaya.

Lakini Kamishina wa wahamiaji wa Umoja wa Ulaya Dimitris Avramopolous aliukataa ukosoaji huo. "Sikubaliani nao," alisema Avramopolous, alipozungumza na gazeti la Funke. Alisema, mapendekezo ya Seehofer hayatakiwi kutenganishwa na jitihada nyingine zinazohusiana na wakimbizi zinazofanywa na Ulaya.