Ujerumani yakataa kushinikizwa na Taleban | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.07.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani yakataa kushinikizwa na Taleban

Ujerumani inashikilia kuwa haitashinikizwa kutimiza madai ya Taliban ya kuondoa majeshi yake nchini Afghanistan.Kauli hiyo inatolewa baada ya raia wawili wa Ujerumani kutekwa jumatano iliyopita pamoja na raia wengine 5 wa Afghanistan.

Gari lililombeba raia wa Ujerumani aliyeuawa

Gari lililombeba raia wa Ujerumani aliyeuawa

Kwa mujibu wa msemaji wa Taliban watu hao wameuawa kwani Ujerumani na Afghanistan wameshindwa kufanya mazungumzo kabla muda wa mwisho uliowekwa kuisha.Wapiganaji wa Taleban nchini Afghanistan wanadai kuondolewa kwa vikosi vya Ujerumani nchini humo.

Kansela Angela Angela Merkel wa Ujerumani anashikila kuwa kukubali shinikizo ni kutowajibika.Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Martin Jaeger raia mmoja wa Kijerumani alikufa kwasababu ya hali aliyokuwamo wakati alipotekwa.Mwili wa mhandisi huyo wa ujenzi ulikuwa na majeraha ya risasi wakati ulipohamishwa hadi hospitali moja mjini Kabul.

Chanzo cha kifo chake bado hakijulikani.Frank-Walter Steinmeir ni waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani na alisema wanatia juhudi.

''Wakati huu maiti inarejeshwa hapa Ujerumani na uchunguzi utafanyiwa hapa.Tunataka kujua chanzo cha kifo na tuna matumaini kwamba habari hizo tutazipata hivi karibuni.Bila shaka tunatia juhudi zaidi ili raia wetu aliyesalia kuachiliwa.Tunawasiliana na serikali ya Afganistan na tunatumai tutafanikiwa''

Duru za wizara ya mambo ya ndani ya Afghanistan kwa upande wake zinaeleza kuwa mmoja wa raia 5 wa Afghanistan aliachiliwa huru ili kuwasilisha mwili huo.

Wakati huohuo waasi wa Taleban nchini Afghanistan wameongeza muda wa mwisho kwa siku moja kabla kuwaua mateka 23 wa Korea Kusini iwapo madai yao hayatatimizwa.Mateka hao walikamatwa alhamisi iliyopita walipokuwa kwenye msafara wa basi kuelekea eneo la kusini mwa Kandahar linaloliunganisha na mji wa Kabul.Ni katika eneo hilo ndiko kulikoanzishwa kundi la Taleban.

Wapiganaji wa Taleban wamewapa hadi mchana wa leo ili kuondoa majeshi yake nchini Afghanistan vilevile kuwaachia wafungwa wake 23 .Mateka hao ni wafuasi wa kanisa la Saemmul kwenye eneo la Bundang,lililoko nje ya mji mkuu wa Seoul.Wengi wao ni manesi na waalimu wa lugha ya Kiingereza walio na umri wa miaka 20 hadi 30.

Hata hivyo inaripotiwa kuwa majadiliano ya kujaribu kuwashawishi kundi la Taleban kuwaachia mateka hao yanaripotiwa kutoendelea vizuri.Kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo Yusuf Ahmadi aliyezungumza na shirika la habari la AFP huenda wakatimiza madai yao ya kuwaua ifikapo jioni.

Kulingana na kiongozi huyo ujumbe wa serikali ya Afghanistan katika mazungumzo hayo hauna madaraka kamili ya kuwaachia wafungwa wa Taleban.

Wakati mazungumzo ya kutafuta suluhu yanaendelea wapiganaji wa Taleban wanaripotiwa kuzingira kundi la mateka hao 70 kwenye eneo la Qarabagh mkoani Ghazni.Ujumbe wa maafisa wanane wa serikali ya Korea kusini wakiwemo naibu waziri wa mambo ya nje na mshauri wa rais wanashiriki katika mazungumzo hayo.

Kulingana na vyombo vya habari vya Korea kasisi wa kanisa la Saemmul lililopeleka watu hao 23 anatangaza kusimamisha shughuli nchini Afghanistan na kuomba radhi kwa jamii zao.Korea Kusini inapiga marufuku raia wake kuzuru nchi ya Afghanistan.

 • Tarehe 23.07.2007
 • Mwandishi Mwadzaya Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHAj
 • Tarehe 23.07.2007
 • Mwandishi Mwadzaya Thelma
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHAj

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com