1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yagawika juu ya kuikabili Iran

30 Julai 2019

Vyama vya kisiasa Ujerumani vinatafautiana kuhusu kuunga mkono ujumbe wa kijeshi uliopendekezwa na Uingereza kwa ajili ya kuzilinda safari za meli katika eneo la Ghuba baada ya meli ya Uingereza kutekwa na Iran

https://p.dw.com/p/3MxXc
Paul-Loebe-Haus Berlin Einschwörung AKK
Picha: Reuters/H. Hanschke

Iran bado iko kwenye mvutano na nchi za Magharibi kuhusu kutekwa kwa meli ya Uingereza.Nchini Ujerumani serikali ya muungano imegawika kuhusu ikiwa ichangie katika ujumbe uliopendekezwa na Uingereza wa kuzilinda safari za meli katika mlango bahari wa Hormuz. Chama cha Social Democrat kinasema hatua za kijeshi zinaweza kuuongeza makali mgogoro huu.

Serikali ya Ujerumani inapambana kutafuta mwelekeo wa wazi kuhusu ikiwa ishiriki katika ujumbe wa kijeshi wa Ulaya utakaoshiriki kwenye harakati za kulinda safari za majini katika mlango bahari wa Hormuz. Ujumbe huo ulipendekezwa na serikali ya Uingereza wiki iliyopita kwa lengo la kuanzisha ujumbe wa pamoja wa nchi zote za ulaya wa kuzilinda safari za meli kwenye eneo hilo la Ghuba wakati Iran na Uingereza kila mmoja akiwa ameishikilia meli ya mwenzake katika kipindi cha wiki za karibuni.

Norbert Röttgen afisa wa ngazi ya juu katika chama cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU pamoja na mwenyekiti wa kamati ya bunge inayohusika na  masuala ya mambo ya nje  anasema kwamba Ujerumani inawajibu wa kimaadili kujihusisha na ujumbe huo na hasa kwa kuzingatia uchumi wa nchi hiyo unaotegemea biashara ya kusafirisha bidhaa nje.

Iran | Britischer Tanker Stena Impero
Picha: picture-alliance/Photoshot/ISNA/M. Akhoundi

Röttgen ameiambia Dw kwamba maendelea ya nchi hiyo yanategemea usafirishaji na kwahivyo nchi inalazimika kuweka wazi msimamo wake kwamba inasimama bega kwa bega na marafiki wa Uingereza,na washirika wake.

Kwa bahati mbaya kuna tafauti za msingi katika sera za Iran na Marekani na ndio sababu Ujerumani haiwezi tu kushirikiana na Marekani bila kutafakari. Hata hivyo chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democratic SPD ambacho kinaunda serikali ya mseto wa CDU/CSU na ambacho kinaishikilia wizara ya mambo ya nje kwa sasa kupitia waziri Heiko Maas kimezidi kuwa na tahadhari. mwanachama wa SPD aliyeko kwenye kamati ya ulinzi bungeni ameiambia DW kupitia barua pepe kwamba hapana shaka kuzilinda njia za biashara huru ni hatua muhimu sana lakini anaamini kwamba hilo linaweza kufanyika kupitia njia za kidiplomasia.Chama cha SPD kinaamini kuzitumia njia za kijeshi kunaweza kukachangia zaidi ukosefu wa usalama.

Iranische Soldaten in der Straße von Hormus
Picha: picture-alliance/XinHua/A. Halabisaz

Kutoka Iran kwenyewe mkanda mwingine wa video na sauti uliotolewa jana umeonesha afisa wa jeshi la mapinduzi la Iran akitowa vitisho dhidi ya wanajeshi walioko kwenye  meli ya kivita ya Uingereza akisema meli hiyo isijaribu kuingilia kati au kuhatarisha maisha.Vidio hiyo pia inajumuisha picha zinazoaminika kwamba huenda zilichukuliwa siku ya tukio la  Julai 19 la kutekwa kwa meli ya Stena Impero iliyokuwa na bendera ya Uingereza.Mkanda huo wa vidio umeonesha malumbano yaliyotokea kati ya wanajeshi wa majini wa Uingereza na walinzi wa Iran wakati wa kukamatwa meli hiyo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Josephat Charo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW