1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaanza uhusiano mpya na Irak

Charo Josephat 18 Februari 2009

Waziri Steinmeier akutana na viongozi wa Irak mjini Baghdad

https://p.dw.com/p/GwX3
Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier (kushoto) na waziri mkuu wa Irak Nouri al-Maliki (kulia)Picha: AP

Ziara ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, mjini Baghdad, imeashiria mwanzo wa mabadiliko ya sera ya Ujerumani nchini Irak. Akiwa waziri wa kwanza wa mambo ya kigeni kuitembelea Irak tangu miaka 22 iliyopita, waziri Steinmeier, amefanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo katika juhudi za Ujerumani kuinyoshea Irak mkono wa urafiki.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amekutana na rais wa Irak, Jalal Talbani, waziri mkuu wa hiyo, Nuri al Maliki na waziri wa kigeni, Hoshyar Zebari, siku ya Jumanne. Zebari amesema baadaya mkutano huo kuwa ziara ya waziri Steinmeier na kusainiwa mikataba kati ya Ujerumani na Irak kunadhihirisha azma ya kuendeleza na kuimarisha uhusinao wa kihistoria kati ya nchi hizo mbili.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, anasema Ujerumani inataka kusaidia kuleta tena matumaini kwa Wairaki na kuacha uaminifu mpya ukue.

"Uchaguzi umedhihirisha kwamba Irak iko katika mchakato wa kuwa imara, hatutaki kusema maneno matamu. Hali ya usalama katika maeneo mengi kama ilivyokuwa hapo zamani bado ni tete, lakini naamini hatua muhimu zimepigwa na ndio maana huu ni wakati unaofaa kwa sisi kujiingiza zaidi nchini Irak, kisiasa na pia kiuchumi."

Ujerumani inakaribishwa sana nchini Irak na ni mshirika katika uchaguzi wa kwanza. Hayo ndiyo aliyoyasikia waziri Steinmeier katika ziara yake mjini Baghdad wakati alipokutana na rais wa Irak, Jalal Talabani, waziri mkuu Nuri al Maliki na waziri wa mambo ya kigeni wa nchi hiyo, Hoshyar Zebari. Kwa mujibu wa viongozi wa kisiasa wa ngazi ya juu, Irak inahitaji ushirikiano na Ujerumani, hususan ufundi wa kisasa wa kampuni za Ujerumani zinazotaka kufanya biashara na Irak. Waziri Steinmeier anasema serikali ya Ujerumani mjini Berlin inainyoshea mkono wa heri Irak mpya.

"Kisiasa tunakaribishwa sana hapa kwa sababu viongozi wa Irak wanajua ni mambo gani mengi yanayohitaji kufanywa katika kuijenga upya miundombinu. Ujerumani inaweza kuwa na msaada mkubwa katika kazi hiyo. Tumekaribishwa sana na tumeulizwa kujenga mfumo wa afya hapa Irak. Hayo ndiyo maswala ambayo msaada wa Ujerumani unakaribishwa, lakini pia katika mtizamo wa kiuchumi."

Mada ya pili tete katika kujenga ushirikiano kati ya Ujerumani na Irak ni utamaduni na ushirikiano katika elimu. Wataalamu wa Ujerumani na wasimamizi wa majumba ya makumbusho watasaidia kulinda utamaduni wa Irak. Mpango wa msaada wa masomo kwa wanafunzi wa Irak unatakiwa kusaidia kujenga upya msingi wa elimu nchini Irak.

Christian Bode, katibu mkuu wa shirika la elimu la Ujerumani, DAAD, anasema, "Inachohitaji Irak baada ya miongo hii miwili ya machafuko makali, yaliyoathiri pia mfumo wa elimu, kuwalazimu vijana wenye akili pamoja na wanasayansi kuikimbia nchi, ni juhudi kamilifu za kuijenga upya. Na juhudi hizi lazima zianze kuanzia nchini."

Mwanzoni kabisa kila mwaka mamia ya wataalamu vijana wa Irak wataweza kusoma katika vyuo vikuu vya Ujerumani. Idadi inaongezeka kwa kuwa idadi ya watu wanaotaka kushiriki kwenye mpango huu ni kubwa mno. Wanafunzi wawili wa kwanza tayari wamepokea ahadi zao siku ya Jumanne.

Waziri Steinmeier ametangaza kufunguliwa kampuni kubwa za Ujerumani za Siemens na Mercedes Benz mjini Baghdad, pamoja na mipango ya kufungua chuo kikuu cha Ujerumani nchini Irak.