Ujerumani na Tanzania zajizatiti kuilinda Selous | Masuala ya Jamii | DW | 19.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Ujerumani na Tanzania zajizatiti kuilinda Selous

Serikali za Tanzania na Ujerumani kwa pamoja zimezindua programu ya utunzaji wa mazingira na maendeleo katika hifadhi ya taifa ya Selous, SECAD, nchini Tanzania.

Hii ni miongoni mwa harakati za pamoja za mataifa hayo na asasi zisizo za kiraia za kutunza hifadhi hiyo na kukabiliana na vitisho vinavyoweza kuondoa hadhi yake kama moja ya eneo la kihistoria za turathi za dunia. 

Makubaliano hayo yalifikiwa Ijumaa iliyopita kati ya Waziri wa maliasili na utalii wa Tanzania Jumanne Maghembe na balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke. Programu hiyo inafadhiliwa na benki ya maendeleo ya Ujerumani ya KfW kwa niaba ya serikali ya Ujerumani na itatekelezwa na wizara ya maliasili na utalii, kwa kushirikiana na mamlaka ya hifadhi za wanyamapori, taasisi ya kimataifa ya hifadhi za uoto wa asili, WWF na asasi inayojihusisha na bustani za wanyama ya Frankfurt, FZS.

Waziri Maghembe alipozungumza kwenye uzinduzi huo uliofanyika kwenye eneo la Matambwe katika hifadhi ya Selous, amesema wanaukubali kwa kiasi kikubwa mpango huo wa serikali ya Ujerumani wa kulinda hifadhi hiyo. Alisema, hatua hiyo inatokana na mpango huo kuwa na msingi imara wa kulinda rasilimali za asili kwa faida ya taifa hilo na urithi wa asili kwa Tanzania.

Tanzania Elefant (Irene Quaile)

Hifadhi ya Selous ina ukubwa wa Skwea Kilomita 50,000

Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania, Egon Kochanke aliongeza kwamba kwa kuzingatia changamoto zinazokabili hifadhi hiyo ya wanyama kama vile uwindaji haramu, lakini pia kwa kuzingatia ukubwa wake na umuhimu wa hifadhi hiyo ya kipekee, serikali ya Ujerumani imejizatiti kuisaidia Tanzania kuilinda hifadhi ya Selous kwa faida ya kizazi cha sasa ni kijacho.

Serikali ya Ujerumani inatoa Euro Bilioni 18 kwa ajili ya uendeshaji wa programu hiyo itakayotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano. Masuala muhimu katika utekelezaji wake ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa hifadhi hiyo.

Washirika wengine kwenye mpango huo FZS na WWF wamekubaliana kusaidia kutoa michango ya kifedha kiasi cha Euro 400,000 kwa kila taasisi. Wakati FZS itahusika zaidi na shughuli zinazofanyika ndani ya hifadhi kwa kusaidiana na mamlaka ya hifadhi za wanyamapori ya Tanzania, utekelezaji wa sheria, ulinzi wa kizazi cha wanyama wanaopewa kipaumbele, na ufuatilizi wa utunzaji wa mazingira, WWF yenyewe itajihuisha na ushauri kwenye idara ya usimamizi wa hifadhi wa namna ya kufikia jamii na uhifadhi, pamoja na shighuli muhimu zinazolenga kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali asilia katika maeneo yanayopewa kipaumbele katika hifadhi hiyo.

Hifadhi ya Selous ni moja ya hifadhi kubwa zaidi Barani Afrika ambayo pamoja na masuala mengine, inatoa vibali vya uwindaji katika baadhi ya maeneo ndani ya hifadhi hiyo. Ina ukubwa wa takriban Skwea Kilomita 50,000, na lilipewa hadhi ya turathi ya dunia, na shirika la kimataifa la turathi, UNESCO mwaka 1982 kutokana na umuhimu wake kimataifa.

mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com