Ujerumani na hali ilivyo Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani na hali ilivyo Afghanistan

Hisia za wanasiasa wa Ujerumani juu ya Afghanistan

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan akipiga kura katika uchaguzi wa mwishoni nchini Afghanistan

Rais Hamid Karzai wa Afghanistan akipiga kura katika uchaguzi wa mwishoni nchini Afghanistan

Baada ya kujiondoa Abdullah Abdulla kutoka duru ya pili ya kinyanganyiro cha kuwania urais wa Afghanistan, tume huru ya uchaguzi katika nchi hiyo imeufuta uchaguzi uliopangwa kufanywa jumamosi ijayo. Kwa hivyo, rais wa zamani na mpya wa Afghnaistan, ni Hamid Karzai, ambaye analalamikiwa kwamba katika duru ya mwanzo ya uchaguzi alifanya udanyifu mkubwa.

Rais wa zamani na mpya Hamid Karzai itambidi ajitahidi kuwa rais wa Wa-Afganistan wote na ayaweka pamoja makambi mbali mbali ya kisiasa katika nchi hiyo. Hayo yalisemwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, baada ya kufutwa duru ya pili ya kinyanganyiro cha uchaguzi wa urais katika nchi hiyo. Uchaguzi wa Aghnaistan uliogubikwa na mizengwe ulionekana hapa Ujerumani kama onyo, nalo ni kwamba bado kunakosekana utawala wa sheria na taasisi zilizo thabiti katika nchi hiyo ambazo zinaweza kuaminiwa na raia. Kwa hivyo, jamii ya kimataifa inabidi ijitiahidi sana katika suala hilo. Watu wanauliza katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin, vipi matatizo ya Afghanistan yanaweza kutanzuliwa, kutoka kwenye mizizi yake, ikiwa viongozi wa nchi hiyo ni mafisadi? Mwanasiasa wa chama cha kiliberali cha Free Democratic, FDP, Werner Hoyer, ana hisia za mchanganyiko kutokana na matukeo ya uchaguzi huo:

Dr. Werner Hoyer

Dr. Werner Hoyer, msemaji wa masuala ya kigeni wa Chama cha FDP hapa Ujerumani

"Nafikiri jamii ya kimataifa duniani ambayo inaendesha harakati zake huko Afghanistan itabidi iliangalie kwa makini suala la utawala wa sheria. Kwa muda, mambo hayatakuwa mazuri kutokana na suala la sasa la namna uchaguzi ulivofanyika, na pia katika wakati ambapo ulaji rushwa na uhalifu wa mpangilio umeikumba nchi hiyo. Haitowezekana kuunda taasisi za dola zinazotegemewa pamoja na dola isiokuwa na ufisadi, hivyo kuwapa imani wananchi wajihusishe na dola yao wenyewe."

Vivyo hivyo ndivyo anavohisi mbunge Tom Koenigs wa Chama cha Kijani, ambaye katika mwaka 2006 na 2007 alikuwa mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Afghanistan:

"Matokeo bila ya shaka ni ya kuvunja moyo, kwa vile huko Afghanistan sasa kuna rais ambaye uhalali wake umeharibika. Pia utaratibu wa uchaguzi umeharibika na imani kwa demokrasia, bila ya shaka, haitokuwa na nguvu zaidi."

Rais aliye dhaifu zaidi na na ambaye uhalali wake umepungua hawezi kuwa ni kwa maslahi ya jamii ya kimataifa, kwa vile serekali ya Rais Hamid Karzai ndio mshirika mkubwa wa kuzungumza nayo wakati wa kufikia makubaliano juu ya malengo ya kuijenga upya nchi hiyo. Jambo hilo linafaa lifanyike mbele ya mkutano wa kimataifa juu ya Afghanistan na ambao umepangwa kufanywa mwanzoni mwa mwakani.

Msemaji wa wa serekali ya Ujerumani, Ulrich Wilhelm, alisema:

" Sisi mwakani tunataka pamoja na serekali mpya itakayoundwa huko Afghanistan kuweka malengo ya kuijenga upya nchi hiyo, kwa mfano, kuboresha mafunzo watakayopewa wanajeshi na polisi. Kutokana na mitihani mikubwa ambayo Afghanistan na pia jamii ya kimataifa iko mbele yao, serekali ijayo inahitaji iungwe mkono na kupata imani ya wananchi wa Afghanistan."

Ukubwa gani uungaji mkono huo, ni jambo ambalo limefunikwa na tetesi.

Kwa sasa serekali ya Ujerumani haijabdilisha msimamo wake kuhusu kuweko jeshi la nchi yake huko Afghanistan. Idadi ya wanajeshi hao, ambayo sasa ni 4,500, na mipango ya kuwaweka wanajeshi hao, haitobadilika pale kibali cha kuweko wanajeshi hao huko Afghanistan kitakaporefushwa hapo Disemba mwaka huu. Uwezekano wa kuengeza idadi ya wanaheshi hao litabidi jambo hilo liamuliwe baada ya mkutano wa kimataifa juu ya Afghanistan.

Kinyume na mtangulizi wake, Franz-Josef Jung wa Chama cha Christain Democratic, waziri mpya wa ulinzi, Karl-Theodor Guttenberg wa Chama cha Christian Social, anazungumzia juu hali zinazofanana na vita huko Afghanistan. Anamfahamu kila mwanajeshi ambaye anasema: Afghanistan kuna vita, alisema Guttenberg katika gazeti la BILD-Zeitung. Mtangulizi wake alijiepusha kutumia neno Vita kuhusiana na harakati za jeshi la Ujerumani huko Afghanistan.

Mwandishi: Wekhäuser, Nina/ZP

Miraji Othman

Mhariri:M.Abdul-Rahman

 • Tarehe 03.11.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KMcu
 • Tarehe 03.11.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KMcu
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com