Ujerumani ilisikiliza simu ya Erdogan | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.08.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ujerumani ilisikiliza simu ya Erdogan

Uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki unaonekana kuyumbishwa baada ya uchunguzi kubaini kuwa shirika la kijasusi la Ujerumani limekuwa likisikiliza mazungumzo ya simu ya baadhi ya wanasiasa wa Uturuki.

Serikali ya Uturuki ilisubiri siku mbili kabla ya kutoa tamko juu ya kashfa ya udukuzi unaosemekana kufanywa na Ujerumani. Leo hii, wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ilimwamuru balozi wa Ujerumani kwenda wizarani kutoa maelezo juu ya kisa hiki. Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Ahmed Davutoglu amesema tabia ya Ujerumani haikubaliki na wala haisameheki. Aliongezea kwamba Ujerumani lazima isimamishe vitendo vya udukuzi mara moja. Davutoglu, ambaye huwenda akawa waziri mkuu baada ya Recep Tayyip Erdogan kuondoka madarakani, amepanga kuzungumza na mwenzake wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.

Hata hivyo, wawakilishi wengine wa serikali ya Uturuki wamekaririwa na gazeti la Cumhuriyet wakisema kuwa hawataki kuutibua zaidi mzozo huu. Wanasiasa hao wanaeleza kuwa hawakushangazwa kuona kuwa shirika la kijasusi la Ujerumani linasikiliza simu za wanasiasa kama Erdogan. Kwa mtazamo wao, hilo ni jambo la kawaida kati ya mataifa mbali mbali, hata kama mataifa hayo ni washirika wa karibu.

Hiki si kisa cha kwanza

Waziri mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan

Recep Tayyip Erdogan amechaguliwa kuwa rais wa Uturuki

Lakini licha ya hayo, kisa hiki kitauathiri uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki. Onur Öymen aliyekuwa balozi wa Uturuki hapa nchini anasema uaminifu kati ya nchi hizo mbili umepungua na kwamba udukuzi wa Ujerumani umeathiri ushirikano baina yao. Öymen anafananisha kisa hiki na kashfa ya udukuzi kati ya Ujerumani na Marekani.

Hii si mara ya kwanza kwa tukio kama hili kutokea baina ya Ujeurmani na Uturuki. Mwaka 2002, wafanyakazi wa mashirika ya kisiasa ya Ujerumani nchini Uturuki walifikishwa mahakamani kwa shutuma za kufanya kazi za kijasusi. Kwa upande mwininge, wafanyakazi 15 wa shirika la kijasusi la Uturuki waliamriwa kuondoka Ujerumani baada ya kukutwa na kosa la kuwatishia wanasiasa wa upande wa upinzani.

Wachambuzi wengi wanaona kwamba nchi za Ujerumani na Uturuki zinaweza kumaliza tofauti zao. Badala ya kuchunguzana, nchi hizo zinaweza kufanya mazungumzo. Lakini wachambuzi hawatarajii kwamba shughuli za ujasusi zitasimamishwa.

Mwandishi: Thomas Seibert

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com