Uhuru wa vyombo vya habari Magazetini | Magazetini | DW | 03.05.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Uhuru wa vyombo vya habari Magazetini

Siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari, mazungumzo kati ya kansela Angela Merkel na rais Vladimir Putin wa Urusi na kashfa inayolitikisa jeshi la shirikisho Bundeswehr ni miongoni mwa mada magazetini

Tunaanza na siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari. Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanakubaliana uhuru wa vyombo vya habari ni mmojawapo wa mihimili muhimu ya demokrasia. Gazeti la "Kieler Nachrichten" linaandika: "Waandishi habari hawapaswi kuachia washawishiwe na hisia au chuki dhidi ya wengine. Jukumu letu ni kukusanya habari zenye uhakika na kuzitathmini. Kuchunguza kwa makini kama habari hizo zina ukweli. Na sio kurukia tu. Uhuru wa vyombo vya habari ni uhuru wa kuripoti au wa kutoripoti. Anayeuhifadhi uhuru huo basi anasadia pia kuhifadhi demokrasia."

Uhuru wa vyombo vya habari una thamani na haulipiki

Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linahoji uhuru wa vyombo vya habari si pambo. Gazeti linaendelea kuandika: "Kazi ya uandiishi habari bila ya mchujo inasalia kuwa mhimili muhimu wa demokrasia. Na hata kama vyote viwili vinaweza kuwa na walakin hata hivyo vinabainisha na kuhakikisha uhuru ambao hauna mfano na haulipiki."

Mazungumzo ndio njia muhimu ya kusaka ufumbuzi

Kwa mara ya kwanza baada ya kupita zaidi ya miaka miwili, kansela Angela Merkel amekutana na rais wa Urusi Vladimir Putin katika mji wa mwambao wa Sotchi. Hata kama misimamo yao inatofautiana, sio tu kuhusu mzozo wa Ukraine bali pia vita nchini Syria, hata hivyo viongozi hao wanakubaliana juu ya umuhimu wa kuendelea kujadiliana. Gazeti la "Sächsische Zeitung" linaandika: "Kusaka ufumbuzi wa mizozo si kazi rahisi. Na mwenye kudai ridhaa ya upande mmoja, hawezi kufika mbali. Ukweli huu unaihusu Ukraine sawa na unavyohusiana na vita nchini Syria. Ingawa kama kansela amefanya la maana alipowakumbusha viongozi wa Urusi kuhusu jukumu lao kama mshirika katika vita, hata hivyo angefanya vizuri pia kuwakumbusha viongozi wa Uturuki, Marekani na Saudi Arabia wanaochangia pia katika balaa linaloendelea nchini Syria."

Jeshi la shirikisho Bundeswehr lakumbwa na misuko suko

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu kashfa inayolitikisa jeshi la shirikisho Bundeswehr. Kumekuwa na ripoti kuhusu siasa kali za mrengo wa kulia miongoni mwa baadhi ya wanajeshi, kashfa za ngono na mateso wakati wa zoezi la kuwasajili wanajeshi. Waziri wa ulinzi bibi Ursula von der Leyen anaukosoa uongozi jumla wa jeshi. Wahariri wanajiuliza kuna nini? Gazeti la Schleswig-Holsteinische Landeszeitung linaandika: "Lawama anazotupiwa von der Leyen hazitomalizika mnamo siku zinazokuja. Na hasa miongoni mwa wanajeshi yadhihirika  watu wamepoteza imani kufuatia lawama za jumla jamala. Anawezaje mwanajeshi aliyepelekwa Mali au Afghanistan kuonyesha mfano mzuri ikiwa nyumbani analaumiwa tena si na mwengine bali na kiongozi wake mwenyewe? Miaka ya nyuma mawaziri wa ulinzi walikuwa wakienziwa sana katika jeshi la shirikisho. Tunawaeza kumtaja kwa mfano Peter Struck wa kutoka chama cha SPD au Karl-Theodor zu Guttenberg wa chama cha CSU licha ya kashfa ya kughushi shahada ya uzamili. Von der Leyen, baada ya yale aliyoyasema mwishoni mwa wiki, anaweza kutajwa kuwa waziri asiyependwa kabisa katika historia ya mawaziri wa ulinzi wa shirikisho la jamhuri ya Ujerumani.

Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Josephat Charo