1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump kukutana na Netanyahu kujadili amani ya Gaza

Amina Abubakar dpa/reuters
29 Desemba 2025

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kushinikiza kuendelea kwa mchakato wa makubaliano ya amani ya Ukanda wa Gaza, wakati atakapokutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu huko Florida.

https://p.dw.com/p/565R7
Israel Jerusalem 2025 | Donald Trump na Benjamin Netanyahu
Rais wa Marekani Donald Trump akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Evan Vucci/REUTERS

Rais Donald Trump alimualika Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika makaazi yake ya kifahari ya Mar-a-Lago Florida, kujadili awamu inayofuata katika mpango wa amani ya Ukanda wa Gaza. Awamu ya kwanza imeendelea kutekelezwa tangu Oktoba 10, baada ya pande hasimu Israel na Hamas kuukubali mpango wa vipengele 20 wa Trump wa kumaliza vita vya zaidi ya miaka miwili katika Ukanda huo wa Gaza.

Hata hivyo imekuwa vigumu kufanikisha awamu ya pili ya mpango huo inayojumuisha Hamas kuweka chini silaha zake, na hatua ya kupeleka kikosi cha kimataifa cha kutuliza hali Gaza. Hamas tayari imepinga shinikizo la kuachia silaha zake. Katika ziara hiyo ya Marekani, Netanyahu ameambatana na wazazi wa mateka wa mwisho wa Israel Ran Gvili, ambae mwili wake bado unashikiliwa na Hamas huko Gaza.

Huku hayo yakiarifiwa Israel bado haijafungua kivuko cha Rafah, kinachounganisha Gaza na Misri ambayo pia ni moja ya matakwa ya mpango wa amani wa Trump. Israel imerejea kusema kwamba itafungua kivuko hicho baada ya kupokea mwili wa Gvilli.

Wachambuzi: Netanyahu hana budi kufanya anachotaka Trump

Kama sehemu ya makubaliano ya usitishaji vita, Hamas iliridhia kutoa miili ya mateka wote waliochukuliwa wakati wa shambulizi la Oktoba 7 2023,  na Israel nayo ilitakiwa kuwaachia baadhi ya wafungwa wa Kipalestina pamoja na miili inayozuiliwa na Tel Aviv. Kwa hiyo chini ya makubaliano hayo, awamu ya pili ya makubaliano inaweza tu kutekelezwa baada ya mateka wote walio hai na waliokufa kurejeshwa Israel.

Israel Jerusalem 2025 |  Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu Picha: Abir Sultan/Pool/AFP/Getty Images

Chuck Freilich mtalaamu wa kisiasa katika chuo kikuu cha Tel Aviv amesema kutokana na Israel kutarajiwa kushiriki uchaguzi mkuu mwezi Oktoba mwakani, Netanyahu anakabiliwa na kibarua kigumu. Amesema Netanyahu hataki malumbano na Trump katika mwaka wa uchaguzi. Ameongeza kuwa Trump anataka kusonga mbele na Netanyahu hana budi kufanya anachokitaka rais huyo wa Marekani.

Trump na Netanyahu ambao wanakutana kwa mara ya sita mwaka huu wanatarajiwa pia kuijadili Iran, ambayo Israel inadai kuwa inaongeza akiba yake ya makombora baada ya makabiliano makali kati ya mataifa hayo mawili katikati ya mwezi Juni mwaka huu.

Katika majadiliano yao, viongozi hao wawili pia watazungumzia migogoro ya Lebanon na Syria huku Marekani ikiwa mpatanishi mkuu katika juhudi za Israel kuwa na makubaliano ya kiusalama na majirani zake hao wa upande wa Kaskazini.

Masaibu yasiyoisha kwa watu wa Gaza