1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Mabaki tuliyokabidhiwa na Hamas sio ya mateka wetu

Amina Abubakar ap/afp/reuters/dpa
3 Desemba 2025

Israel imesema matokeo ya uchunguzi wa mabaki yaliyorudishwa kutoka Gaza sio ya mateka wake waliouwawa na Hamas, huku pande zote mbili zikiendelea kutekeleza makubaliano dhaifu ya kusitisha vita katika Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/54fwn
Israel Jerusalem 2025 | Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mabaki yaliyokabidhiwa na Hamas sio ya mateka wa taifa hilo walioshikiliwa na Hamas mjini GazaPicha: Ohad Zwigenberg/AFP

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu imesema imefikia uamuzi huo kufuatia uchunguzi wa vinasaba uliofanwa kwa mabaki hayo. Taarifa hizo zilitolewa kwa Jamaa wa mateka wawili waliouawa ambao miili yao bado ipo katika Ukanda wa Gaza.

Mateka hao walichukuliwa na wanamgambo wa Hamas wakati wa shambulio la Oktoba 7 2023, shambulio lililochochea mgogoro mkubwa, unaoendelea sasa mashariki ya kati. Hata hivyo wanamgambo wa Hamas wamesema tayari mabaki ya mateka mmoja, yamepatikana na tayari serikali ya Israel imefahamishwa na kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu.

Hii si mara ya kwanza mabaki ya mateka yasiyo sahihi kukabidhiwa kwa Israel, matukio kama hayo yaliyoshuhudiwa awali yalisababisha mvutano kati ya Israel na Hamas, huku Israel ikisema Hamas inajikokota katika hatua ya kuirejesha miili hiyo na Hamas nayo ikisema bado, ilikuwa inaitafuta baadhi ya miili iliyoaminika kuwa chini ya vifusi vya majengo yaliyoshambuliwa na Israel, katika Ukanda wa Gaza.

Hadi sasa makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano yanayoungwa mkono na Marekani yamekuwa yakitekelezwa tangu Oktoba 10 kwa lengo la kusitisha vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka miwili.

Qatar kuzishinikiza Israel na Hamas kuanza duru mpya ya mazungumzo

Huku hayo yakiarifiwa Qatar, imesema inatumai pande hizo mbili hasimu, Israel na Hamas wanaweza kurejea katika awamu mpya ya mazungumzo kufikia mpango wa amani ya kudumu katika eneo hilo la wapalestina, kufuatia makubaliano hayo ya Oktoba 10.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed al-Ansari akizungumza na waandishi habari mjini Doha
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed al-Ansari, akisisitiza kwamba wanafikiria kuzishinikiza Israel na Hamas kuingia katika awamu ya pili ya majadiliano ya amaniPicha: Imad Creidi/REUTERS

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Qatar Majed al-Ansari, amesema wanafikiria kuwashinikiza kuingia katika awamu ya pili ya majadiliano hivi karibuni.

"Tunafanya kazi kwa karibu sana, na tunafikiri kwamba tunapaswa kuzishinikiza pande zote kufikia hatua ya pili hivi karibuni. Mambo yanayoendelea huenda yakayumbisha makubaliano yaliyopo. Lakini tunaendelea kujitolea na washirika wetu kusonga mbele zaidi na kuhakikisha kwamba tunapata matokeo chanya na kuelekea katika hatua ya pili."

Akizungumza na waandishi habari mjini Doha Al-Ansari, pia alikosoa mashambulizi ya Israel ya mara kwa mara mjini Gaza, licha ya makubaliano hayo yaliyoongozwa na Marekani, Misri na Qatar yenyewe ya usitishwaji mapigano.

Kwengineko Kitengo cha jeshi la Israel kinachosimamia shughuli za kuratibu utoaji msaada Gaza,COGAT, kimesema Israel itafungua kivuko cha Rafah katika siku chache sijazo, kutoa nafasi ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza kulitoroka eneo hilo na kuingia nchini Misri.

Kwanini Israel inayashambulia majengo Gaza City?