Trump atuma pendekezo la mpango wa amani kwa Iran
25 Machi 2026
Hayo ni wakati Tehran ikitangaza kwamba itaruhusu meli za mafuta "zisizohusika na vita" kupita katika Mlango-Bahari muhimu wa Hormuz. Dalili za awali za suluhu ya kidiplomasia zilijiri licha ya machafuko mapya, huku kombora la Iran likisababisha majeraha nchini Israel ambayo nayo iliendeleza operesheni zake za kijeshi na kuapa kutwaa udhibiti wa ukanda wa kusini mwa Lebanon.
Akizungumza na waandishi Habari katika Ikulu ya White House, Trump alisema Marekani "inafanya mazungumzo hivi sasa" na Iran -- ambayo haijathibitisha kuwepo kwa mazungumzo yoyote rasmi. "Walifanya jambo la kushangaza jana. Walitupatia zawadi na zawadi hiyo ikafika leo. Ilikuwa zawadi kubwa sana, yenye thamani ya kiasi kikubwa cha pesa. Kwa hivyo hiyo ilimaanisha jambo moja kwangu. Tunashughulika na watu sahihi."
Hakuelezea zaidi lakini alisema Zawadi hiyo inahusiana na Mlango-Bahari wa Hormuz, ambao Iran imeufunga kwa kiasi kikubwa ili kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani na Israel, hatua iliyosababisha bei za nishati duniani kupanda.
Iran, katika ujumbe uliosambazwa na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Baharini muda mfupi baadaye, ilitoa hakikisho la kuruhusu "vyombo visivyo vya uadui" kupita salama katika njia hiyo.
Makubaliano ya nyuklia?
Waziri mkuu wa Pakistan amejitolea kuandaa mazungumzo kati ya Marekani na Iran, ambayo Trump alisema yanawahusisha maafisa wakuu akiwemo Makamu wa Rais JD Vance.
Gazeti la New York Times, likiwanukuu maafisa ambao hawakutajwa majina, lilisema Marekani imetuma pendekezo la mpango wa vifungu 15 kwa Iran kupitia kwa Pakistan.
Televisheni ya Israel ya Channel 12 ilisema Trump miongoni mwa mengine, anapendekeza kusitisha mapigano kwa mwezi mmoja ambapo pande hizo zitajadili pendekezo ambalo litajumuisha Iran kukabidhi madini ya urani yaliyorutubishwa na kupiga marufuku urutubishaji zaidi.
Iran imeituhumu Israel kwa kufanya shambulizi la pili kwenye kinu cha nishati ya nyuklia cha Bushehr, kilichoko karibu na vituo vya makaazi ya watu katika Ghuba ya Uarabuni.
- Wanajeshi wako njiani licha ya diplomasia –
Licha ya matumaini ya Trump ya diplomasia, jarida la The Wall Street Journal limeripoti kwamba Marekani inapanga kuwapeleka Mashariki ya Kati wanajeshi 3,000 kutoka Kikosi cha 82 cha Wanajeshi wa Anga.
Makombora ya Iran yamepata mafanikio kwa kupenya mifumo ya ulinzi ya Israel, huku picha za AFP zikionyesha mitaa iliyotapakaa vifusi katika kitovu cha kibiashara cha Tel Aviv.
Israel imesema ilifanya "wimbi kubwa" la mashambulizi ya anga katika maeneo kadhaa ya Iran. Msemaji wa jeshi la Israel Effie Defrin alisema mpango wa vita wa nchi yake "haujabadilika" licha ya matamshi ya Trump na kwamba utaendelea "kusababisha uharibifu na kuondoa vitisho.
Israel pia imeimarisha kampeni yake dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hezbollah linaloungwa mkono na Iran nchini Lebanon, ikisema jeshi lake litachukua udhibiti wa kusini mwa Lebanon hadi eneo la mto Litani, karibu kilomita 30 (maili 20) kutoka mpakani.
Lebanon, ambayo serikali yake kuu imekuwa dhaifu kwa muda mrefu, ilizidi kuwa na msimamo mkali kwa kutangaza kwamba imemwamuru balozi wa Iran kuondoka ifikapo Jumapili, ikiishutumu jamhuri hiyo ya Kiislamu kwa kuingilia masuala ya ndani na kufadhili operesheni za Hezbollah.
Bahrain, Kuwait, Falme za Kiarabu na Saudi Arabia zote zilisema zimezuia mashambulizi mapya ya droni na makombora huku Iran ikiendelea na mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya mataifa ya Ghuba ambayo ni washirika wa Marekani.
AFP, AP, DPA, Reuters