1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aonya kupeleka huzuni Korea Kaskazini

Iddi Ssessanga
8 Septemba 2017

Rais wa Marekani Donald Trump amesema angependelea kutotumia nguvu za kijeshi dhidi ya Korea Kaskazini lakini iwapo atatumia njia hiyo itakuwa siku ya huzuni kwa uongozi wa Pyongyang kwani nguvu ya Marekani ni kubwa mno.

https://p.dw.com/p/2ja5l
USA PK Präsident Donald Trump und Amir al-Sabah
Picha: picture-alliance/abaca/D. Olivier

Rais Trump alikataa kuondoa uwezekano wa hatua za kijeshi dhidi ya Korea kaskazini kufuatia jaribio lake la sita na lenye nguvu zaidi la nyuklia, wakati ambapo utawala wake ukitafuta kuongeza vikwazo vikali zaidi vya kiuchumi, akisema Pyongyang ilikuwa inaonyesha tabia mbaya ambayo inapaswa kukoma.

"Ningependelea kutotumia njia ya kijeshi, lakini bila shaka ni jambo linaloweza kutokea, na kila siku tunapata silaha mpya za nyuklia, natumai hatutozitumia dhidi ya Korea Kaskazini. Ikiwa tutazitumia dhidi ya Korea Kaskazini, itakuwa siku ya huzuni kubwa kwa Korea Kaskazini," alisema Trump.

Nordkorea - Pyongyang feiert die refolgreich getestete Wasserstoffbombe
Wakaazi wa Pyongyang wakisherehekea mafanikio ya jarobio la hydrogen Septemba 2, 2017.Picha: Reuters/KCNA

Hata wakati Trump akisisitiza kuwa huu sasa siyo wakati wa kuzungumza na Korea Kaskazini, maafisa waandamizi wa utawala wake wamebainisha wazi kwamba mlango wa suluhisho la kidiplomasia bado uko wazi, hasa kwa kuzingatia tathmini ya Marekani kwamba shambulio lolote la kuzuwia litasababisha majibu makubwa kutoka Korea Kaskazini.

China, Ujerumani zahimiza suluhu ya amani

Wakati Trump akitoa matamshi makali dhidi ya Korea Kaskazini, China ilikubaliana jana kuwa Umoja wa Mataifa unapaswa kuchukuwa hatua zaidi dhidi ya Pyongyang lakini pia imeendelea kushinikiza majadiliano kusaidia kutatua mkwamo huo.

Na katika mazungumzo hapo jana Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa China Xi Jinping walihimiza njia za amani kutatua mgogoro huo, na kuunga mkono vikwazo vikali dhidi ya taifa hilo baada ya jaribio hilo la nyuklia. Msemaji wa serikali ya Ujerumani Steffen Seibert, alisema jaribio hilo la nyuklia linawakilisha hatari kubwa kwa usalama wa kanda nzima na ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa.

Rais Xi amemuambia rais wa Ufransa Emmanuel Macron leo Ijumaa kuwa anatumai Ufaransa itatoa mchango katika kuanzisha tena mazungumzo kuhusu Korea Kaskazini. Televisheni ya taifa ya China, imesema Xi amesema katik mazungmzo ya simu ya Macron, kwamba suala la rasi ya Korea linaweza kutatuliwa tu kwa njia za amani, ikiwemo kupitia majadiliano, na mashauriano.

Archivbild Kim Jong-Un
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un.Picha: Reuters/KCNA

Macron alisema Ufaransa ilikuwa inafanyakazi kuendeleza amani na utulivu katika rasi hiyo, na kusifu mchango wa China katika kutatua suala hilo, imesema televisheni ya China, CCTV.

Uingereza yataka raia wa Korea Kaskazini kutimuliwa EU

Wakati huo huo, Uingereza imeunga mkono hatua za kufukuzwa kwa wafanyakazi wa Korea kaskazini kutoka Umoja wa Ulaya kama sehemu ya vikwazo vipya kuiadhibu Pyongyang baada ya jaribio hilo la karibuni zaidi. Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson, amesema kuna makubaliano mapana miongoni mwa wenzake wa Umoja wa Ulaya, juu ya kuendelea na vikwazo vipya dhidi ya utawala wa kim Jong Un baada ya kufanya jaribio hilo la Jumapili.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, rtre

Mhariri: Saumu Yusuf