1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aionya Uturuki kuhusu operesheni ya Syria

Bruce Amani
25 Januari 2018

Rais wa Marekani Donald Trump amemtaka mwenzake wa Uturuki Rais Recep Tayyip Erdogan kusitisha operesheni ya kijeshi katika eneo la Kikurdi la Afrin nchini Syria

https://p.dw.com/p/2rU7u
Syrien Von der Türkei unterstützende Syrischen Rebellen
Picha: Getty Images/AFP/N. Al-Khatib

Rais wa Marakani Donald Trump amekuwa kiongozi wa hivi karibuni kumtaka Rais wa Uturuki Tayyip Erdogan kupunguza operesheni ya kijeshi inayofanywa na nchi yake katika eneo la Kikurdi la Afrin kaskazini mwa Syria. Kufuatia miito ya aina hiyo kutoka kwa viongozi wengine wa dunia, Trump alizungumza kwa njia ya simu na Erdogan hapo jana, na kuitaka serikali ya Uturuki kupunguza hatua yake ya kijeshi na kuepusha vifo vya raia.

Taarifa kutoka Ikulu ya White House imesema Trump pia alimuonya Erdogan kuhusu matamshi aliyosema ni ya uharibifu na ya uwongo dhidi ya Marekani ambayo yanatolewa na Uturuki, wakati washirika hao wawili wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wakijikuta katika malumbano kuhusu eneo lililoko karibu na mpaka wa Uturuki ambalo linadhibitiwa na wapiganaji wa Kikurdi wa YPG.

USA Washington - Donald Trump im Oval Office
Trump alizungumzia na Erdogan kuhusu suala la Afrin Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Hata hivyo maafisa wa Uturuki wamepinga taarifa iliyotolewa na White House wakisema haikusema ukweli wa kilichozungumzwa na marais hao wawili. Wamesema Trump hakuzungumzia kuhusu wasiwasi wa kuongezeka kwa machafuko kutokana na operesheni hiyo ya Uturuki.

Pia wamesema kuwa wakati wa mazungumzo hayo ya simu, Rais Trump aliihakikishia Uturuki kuwa Marekani haitawapa tena silaha wapiganaji wa Kikurdi nchini Syria. Uturuki inalichukulia kundi hilo kuwa la kigaidi. Katika matamshi tofauti, Erdogan aliapa kuitanua operesheni hiyo ya kijeshi hadi Manbij, eneo jingine la Wakurdi karibu kilomita 100 mashariki mwa Afrin, ambako wanajeshi wa Marekani wamekita kambi pamoja na jeshi la Kidemokrasia la Syria – SDF. "Operesheni hii itaendelea hadi pale mtu wa mwisho wa kundi hilo la kigaidi ambalo limehifadhi katika eneo hilo magari 5,000 na ndege 2,000 zilizojaa silaha, anamalizwa. Tunaona hilo kuwa ni jukumu letu kuyaangamiza makundi yote ya kigaidi"

Na wakati viongozi hao wawili wakizugnumza, mapigano yaliendelea katika eneo la Afrin nchini Syria, na eneo jirani la Uturuki, ambako maroketi yaliyofyatuliwa kutoka Syria yaliwaua watu wawili na kuwajeruhi wengine 11. Uturuki inaendeleza operesheni hiyo ambayo imeingia siku yake ya sita, ambapo vifaru Zaidi vimepanga foleni kwenye upande wa mpaka wa Uturuki, wakati wanajeshi wakiwa tayari kuingia Syria.

Shirika linalofuatilia matukio ya ukiukaji wa haki za binaadamu la Syria limesema ndege za Uturuki zimeshambulia maeneo ya kaskazini mashariki na kaskazini magharibi mwa Afrin, zikilenga kulirudisha nyuma kundi la YPG na kufungua njia kwa ajili ya mashambulizi ya nchi kavu. Shirika hilo limesma kuna mapigano makali katika eneo hilo kutoka kwa wapigajani wa Kikurdi.

Mwandishi: Bruce Amani/(AFP, AP, dpa, Reuters) http://bit.ly/2rEWJgz
Mhariri: Gakuba, Daniel