1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Terstegen: Tanzania irahisishe upatikanaji wa vibali

20 Machi 2024

Balozi wa Ujerumani, Tanzania, Thomas Terstegen, ameiomba serikali ya Tanzania, kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa vibali vya kazi kwa raia wa Ujerumani wanaofanya kazi Tanzania.

https://p.dw.com/p/4dwpX
Tansania Die Präsidentn von Tansania Samia Suluhu Hassan mit der Staatsminsterin des Auswärtigenamtes Katja Keul
Rais Samia Suluhu akiwa na Waziri wa Ujerumani Katja KeulPicha: Tanzania Statehouse

Terstegen amesema hii itasaidia kuendelea kuimarisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.


Balozi Thomas ameyasema hayo leo katika mkutano wa utiaji saini wa hati za makubaliano ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo uliofanyika leo, jijini hapa.

Mchakato wa upatikanaji Visa urahisishwe


Amesema ili kuwepo kwa ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kuwepo na mfumo rafiki wa upatikanaji wa vibali vya kazi na visa kwani wakati mwingine raia wa Ujerumani hulazimika kurudi Ujerumani hadi pale watakapopata vibali ndipo wanaporudi tena.


"Tunaomba mtusaidie kurahisisha mchakato wa upatikanaji wa visa na kuhakikishautekelezaji wa miradi ya mashirikiano inakwenda kwa urahisi,mwisho wa siku, Tanzania na ujerumani zitapimwa kwa matokeo yake. urahisishaji wa mchkao huo ni kigezo kikuu cha ushirikiano huu," alisema Thomas Terstegen.


Amesema miradi hiyo kwa kiasi inajikita katika kuimarisha haki za binadamu, na utawala bora.


Kadhalika amesema serikali ya Tanzania na Ujerumani zinakwenda kutekeleza miradi zaidi ya saba ya maendeleo ikiwamo utalii, utunzaji wa bayoanuwai, afya, haki za wanawake na watoto na bima ya afya kwa wote.


 Akizungumza katika hafla hiyo ya utiaji saini, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbwa amesema Ujerumani imetoa kiasi cha euro milioni 70, sawa na Shilingi za Kitanzania, bilioni 195.7.


"Tunaomba pande zote mbili zinashirikiana kwa ukaribu ili kuhakikisha miradi iliyotajwa inatekelezwa kwa wakati na ili kufikia malengo ya maendeleo yaliyokusudiwa. Mwisho ningependa kuthibitisha tena dhamira ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wetu wa maendeleo ya watu wetu," alisema Elijah Mwandumbwa.

Ushirikiano utaongeza maendeleo baina ya Tanzania na Ujerumani


Amesema miradi hiyo katika sekta ya afya itajumuisha, huduma za dharura, afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa vijana, usawa wa jinsia, haki za wanawake na kuzuia aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na utawala bora wa fedha.


Marcus Von Essen, Mkuu wa Idara ya Afrika Mashariki, wizara ya ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo ya Ujerumani amesema ushirikiano wa nchi hizi mbili unakwenda kukuza maendeleo na dhamira kuu ni kukuza uhusiano huo kati ya Tanzania na Ujerumani.


Hii si mara ya kwanza kwa ujerumani kuipa Tanzania misaada ya maendeleo, Machi mwaka huu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa ujerumani, katja Keul alizuru Tanzania na miongoni mwa aliyoahidi ni Ujerumani kuipa Tanzania jumla ya Euro 201,130 kwa ajili ya kusaidia katika ukarabati wa jengo la King George V lililopo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni jijini Dar es Salaam na kuandaa onesho la historia ya Tanzania kwa pamoja ambalo litawekwa mjini Berlin Ujerumani na baadaye Tanzania.