Syria yaialika OPCW kuchunguza shambulizi la sumu | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Syria yaialika OPCW kuchunguza shambulizi la sumu

Serikali ya Syria imelialika shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za kemikali, kupeleka ujumbe wa wataalamu wake kuchunguza madai kwamba lilifanyika shambulizi la sumu kwenye mji wa Douma, Ghouta Mashariki.

Shirika la habari la Syria, SANA limeripoti leo kuwa nchi hiyo iko tayari kushirikiana na shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za kemikali, OPCW, kubaini ukweli wa madai hayo na ili liweze kutimiza shughuli zake kikamilifu. Syria pia imelitaka shirika hilo kuendesha uchunguzi wake kwa uwazi pamoja na kuzingatia ushahidi imara na wa kuaminika. Serikali ya Syria na washirika wake wamekanusha kuhusika katika shambulizi lolote la aina hiyo.

Syria katika tahadhari

Syria iko katika tahadhari baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuapa kwamba huenda jeshi lake likachukua haraka hatua za kijeshi kama hatua ya kulipiza kisasi kutokana na shambulizi hilo la sumu, ambalo limekosolewa vikali kimataifa. Marekani, Ufaransa na Uingereza zimeongeza shinikizo kwa serikali ya Syria kwa kuahidi kuchukua hatua kali.

Ufaransa leo imeonya kuwa italipiza kisasi dhidi ya Rais wa Syria, Bashar al-Assad kama ushahidi utaonyesha kuwa shambulizi la sumu lilifanyika katika eneo la Douma ambalo linadhibitiwa na waasi. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema Urusi itapendekeza azimio la Umoja wa Mataifa la kuchunguza madai ya kutumika silaha za sumu Syria, baada ya Urusi kulikataa azimio kama hilo lililopendekezwa na Marekani.

Syrien UN Waffeninspektoren

Timu ya uchunguzi ya UN ikiangalia mchanga karibu na sehemu yalipofanyika mashambulizi ya sumu

''Wawakilishi wa shirika la Hilali Nyekundu nchini Syria na wawakilishi wa Urusi wanaohusika na usalama wa mionzi ya juu ya nishati wamelitembelea eneo ambalo inadaiwa shambulizi lilifanyika huko Douma na hawajapata ishara yoyote ya sumu, kama tulivyosema mara nyingi. Hata hivyo, tunawaalika wataalamu wa OPCW kwenda huko na tutaifanikisha ziara hii,'' alisema Lavrov.

Urusi na Marekani zakinzana

Mapendekezo hayo yanayokinzana kutoka kwa Urusi na Marekani, yanaliweka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika mgongano ambao unaweza kuchochea kupigwa kura za turufu kwa pande zote mbili. Awali, mwanadiplomasia wa baraza hilo alisema Marekani ilikuwa inashinikiza kura ifanyike kuhusu azimio hilo ifikapo leo, lakini hakuna kura yoyote ambayo ilikuwa imeombwa rasmi hadi jana usiku.

Hayo yanajiri wakati ambapo mabasi kadhaa yamewasili kwenye eneo la kaskazini mashariki mwa Syria ambalo linadhibitiwa na waasi likiwa limewabeba wapiganaji wa Syria ambao wamekubali kuusalimisha mji waliokuwa wanaudhibiti karibu na Damascus, baada ya kushambuliwa kwa shambulizi linalodaiwa kuwa la sumu.

Zoezi la kuwaondoa wapiganaji hao pamoja na familia zao, linafanyika wakati ambapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana baadae leo kujadiliana kuhusu shambulizi linalodaiwa kuwa la sumu ambalo lilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo, AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com