Syria iache kutumia mabavu dhidi ya waandamanaji
5 Mei 2011Katibu Mkuu, Ban Ki-moon, ni miongoni mwa viongozi wachache wa kimataifa, kuweza kuzungumza binafsi na Assad kwa njia ya simu, tangu maandamano ya upinzani kuibuka nchini Syria katikati ya mwezi wa Machi. Ban Ki-moon amesema kuwa mageuzi yaliyoahidiwa kufanywa na serikali ya Rais Bashar al-Assad yanapaswa kutekelezwa mapema na kwa ukamilifu. Amesisitiza umuhimu wa kushiriki katika majadiliano yalio wazi na kweli, yakizingatia mchakato wa mageuzi. Rais al-Assad vile vile ashirikiane na tume ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kuchunguza machafuko ya nchini humo.
Syria itazidi kutengwa
Wakati huo huo, Marekani na Italia zimeionya Syria kuwa itakabiliwa na vikwazo vingine na itazidi kutengwa, ikiwa haitoacha kutumia mabavu dhidi ya waandamanaji wanaodai mageuzi nchini humo. Leo, katika mkutano na waandishi wa habari mjini Rome, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton na waziri mwenzake wa Italia, Franco Frattini walisema kuwa serikali ya Syria yapaswa kushinikizwa kukomesha matumizi ya nguvu yaliyosababisha vifo vya mamia ya watu, tangu maandamano ya upinzani kuanza nchini humo. Ripoti zinasema wanajeshi kadhaa pia waliuawa katika machafuko hayo.
Operesheni ya Daraa yakamilishwa
Kwa mujibu wa makundi ya haki za binadamu, zaidi ya watu 600 wameuawa tangu maandamano hayo ya upinzani kuanza nchini Syria tarehe 15 mwezi Machi. Kundi la haki za binadamu la Syria "Insan" linasema,hadi watu 8,000 wameorodheshwa kama wale waliokamatwa au wasiojulikana walipo. Kwa upande mwingine, hii leo televisheni ya taifa ya Syria imesema kuwa wanajeshi wameanza kuondoka katika mji wa kusini wa Daraa, kitovu cha upinzani dhidi ya serikali. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanajeshi wameshakamilisha operesheni yao kwa kuwakamata wale walioitwa "magaidi" na kwamba wamefanikiwa kurejesha utulivu.
Wanajeshi watumiwa kuzima upinzani
Wakati huo huo, mwanaharakati mmoja nchini Syria, ameripoti kuwa zaidi ya watu 300 wamekamatwa katika mji wa Saqba ulio nje ya mji mkuu Damascus, wakati vikosi vya usalama, vikiendelea kutumia nguvu katika jitahada ya kukandamiza upinzani nchini humo. Mwanaharakati huyo ambae hakutaka kutajwa kwa jina, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa vikosi vya usalama vilisaidiwa na wanajeshi. Afisa mmoja wa Kiarabu anaefuatiliza matukio ya nchini Syria, anasema, uamuzi wa Assad kutumia majeshi ni ishara kuwa kiongozi huyo hataki maridhiano.
Mwandishi: Martin,Prema/RTRE/AFPE
Mhariri:Josephat Charo