1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyama vikuu viwili vilisusia uchaguzi huo.

12 Aprili 2010

Uchaguzi huo ni wa kwanza tangu 1986, matokeo kutangazwa tarehe 18 mwezi huu.

https://p.dw.com/p/Mtga
Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan akipiga kura jana mjini Khartoum.Picha: AP

Sudan, ambayo ni nchi kubwa kabisa barani Afrika, kwa kipindi cha miongo miwili imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya sehemu ya kaskazini inayokaliwa na Waarabu na kusini ambapo raia wengi ni Wakristu. Jimbo la magharibi la Darfur pia limekuwa chanzo cha machafuko kutokana na kukithiri kwa mashambulio ya waasi.

Sudan Wahlen Omar al-Bashir
Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter afanya mazungumzo na rais Al-Bashir katika ikulu, KhartoumPicha: AP

Hata hivyo, uchaguzi unaoendelea wa kitaifa umekosa uzito unaostahili kwa sababu vyama viku viwili vya upinzani vimeususia kutokana na kile kilichotajwa kama hujuma kutoka kaskazini. Wachunguzi wa kimataifa awali walikuwa wamependekeza kwamba uchaguzi huo uahirishwe kwa muda kutokana na changamoto za kimsingi hasa kutoka kwa tume ya uchaguzi nchini humo.

Taarifa katika vyombo vya habari nchini Sudan ilisema shughuli ya uchaguzi ilicheleweshwa katika vituo kadhaa vya kupiga kura kutokana na ukosefu wa karatasi za kura na katika maeneo mengine, wapiga kura walikanganywa kutokana na ugumu wa kusoma maelezo, na wengi pia walikosa majina yao katika daftari la majina ya wapiga kura.

Rais Omar al-Bashir ana uhakika wa kushinda kwa kishindo hasa baada ya mahasimu wake kisiasa, Sadiq al-Mahdi wa chama cha Umma, na Yasir Arman wa chama maarufu kusini mwa Sudan cha The Sudan Peoples Liberation Movement, SPLM, kususia uchaguzi huo wa rais.

Sudan Wahlen Kandidat Salva Kiir
Rais Salva Kiir wa Sudan kusini kabla ya kupiga kura, katika eneo la Juba, Sudan kusini.Picha: AP

Salva Kiir, kiongozi wa eneo la kusini anatarajiwa kushinda katika eneo hilo. Wanasiasa hao walidai kwamba wizi wa kura ulikuwa umepangwa na kwamba walikuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa jimbo la Darfur linalokumbwa na ghasia.

Kumekuwa na ukosoaji mkubwa wa uchaguzi wa Sudan hasa kutoka kwa washiriki wa Umoja wa Mataifa, Marekani na mashirika ya kutetea haki za binadam. Hata hivyo, rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter alikiri kwamba Sudan ina matumaini ya mwangaza hasa ikizingatiwa kwamba ilikuwa imezongwa na vita kwa muda mrefu.

Sudan Wahlen Markierung
Raia milioni 16.5 wamejiandikisha kupiga kura Sudan.Picha: AP

Rais al-Bashir aliyeingia madarakani baada ya mapinduzi mwaka wa 1989 anadai kwamba uchaguzi huo ni wa haki. Takriban raia milioni 2.6 ambao ni wakimbizi wanaoishi katika kambi hawajaandikishwa kupiga kura.

Wachunguzi wa kisiasa nchini Sudan wanadai kwamba kuna jitihada za kuhakikisha al-Bashir anasalia madarakani, ingawa anatakiwa kujibu mashtaka ya ukiukaji wa haki za binadamu mbele ya mahakama kuu ya kimataifa ya uhalifu wa kivita. Al-Bashir alitishia mwanzoni kwamba atafutilia mbali kura ya maoni ya mwaka ujao ya ikiwa vyama vya kisiasa vitasusia uchaguzi huo.

Wapiga kura milioni 16.5 wamejiandikisha kupiga kura nchini Sudan. Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa tarehe 18 mwezi huu.

Mwandishi, Peter Moss /DPA / AFP

Mhariri, Othman Miraji