Shirika la afya Duniani WHO latimiza miaka 60 | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Shirika la afya Duniani WHO latimiza miaka 60

Si dunia tu inayoathirika kwa mabadiliko ya hali ya hewa,bali wakaazi wake pia.Hayo tunakumbushwa na Shirika la Afya Duniani WHO likitimiza miaka 60 tangu kuzinduliwa kwake.

Hata baada ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Afya Duniani WHO,bado kuna mengi yanayohitaji kutekelezwa.Kwani kama ilivyokuwa hapo zamani, umasikini bado ni sababu kuu ya magonjwa duniani.Hata katika nchi tajiri kwenye maisha ya hali ya juu,masikini hawana uwezo wa kujipatia matibabu.Na katika nchi zinazoinukia mambo ni mabaya zaidi kwani masikini ndio hawana huduma zozote za afya: wao hawana madaktari,wakunga wala wauguzi.Isitoshe,mabadiliko ya hali ya hewa pia yana athari ambazo hudhihirika wazi wazi.

Kwa hivyo shirika la WHO linatoa mwito wa kuwepo huduma za afya ya kimsingi kwa kila mmoja.Ukweli ni kuwa afya haiwezi kununuliwa kwa pesa,kinyume na matibabu na kinga dhidi ya magonjwa.Kwa mfano katika nchi tajiri na masikini,baadhi ya magonjwa yanaweza kuepukwa,umma unapofahamishwa au kufunzwa mambo kadhaa kama vile kupunguza uzito wa mwili na kuacha sigara ili kujiepusha na maradhi ya moyo,kisukari na kadhalika.Maradhi kama hayo yangeweza kudhibitiwa kwa kufanywa kampeni za kutoa maelezo na ikiwa viongozi pia watakuwa na dhamira ya kuchukua hatua hizo.

Msaada wa kuanzisha huduma za afya ya msingi kwa ajili ya umma katika nchi zinazoendelea,ni sharti kuu la kimsingi ili siasa ya maendeleo iweze kufanikiwa.Kinachohitajiwa ni fedha.Lakini matatizo mapya yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa duniani,ni vigumu zaidi kudhibitiwa.

Kwa hivyo mwaka huu,Shirika la WHO linatoa umuhimu pia kueleza jinsi mabadiliko ya hali ya hewa yanavyohatarisha afya.Ukame,mafuriko na vimbunga ni matokeo ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa yanayozusha matatizo mapya ya afya.Jamii za kimataifa hazina budi ila kushirikiana kutafuta njia za kutenzua matatizo hayo.

Miongoni mwa hatua za kutekelezwa ni kuhakikisha kuwa kila mmoja kote duniani anapatiwa huduma za kimsingi kuhusika na afya.Mifumo ya afya katika nchi zilizo masikini kabisa,isaidiwe na jumuiya ya kimataifa kwani umasikini ni chanzo kikuu cha magonjwa na kifo.Katika ulimwengu wa leo wa utandawazi,kuna njia moja tu ya kupambana na maradhi ya kuambukizwa:ni kupiga vita umasikini kote duniani.

 • Tarehe 07.04.2008
 • Mwandishi H.Jeppesen/P.Martin
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DdCG
 • Tarehe 07.04.2008
 • Mwandishi H.Jeppesen/P.Martin
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DdCG
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com