Merz ashinikiza Wasyria warejee kwao katika ziara ya Sharaa
30 Machi 2026
Katika ziara hiyo, Sharaa alikutana na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier pamoja na kufanya mazungumzo na Kansela Friedrich Merz kuhusu mustakabali wa Syria baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 14.
Baada ya mazungumzo hayo, Merz alisema Ujerumani na Syria zinafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha Wasyria wengi zaidi wanaweza kurejea nchini mwao. Aliongeza kuwa viongozi hao wamekubaliana kuwa asilimia 80 ya Wasyria walioko Ujerumani wanapaswa kurejea ndani ya miaka mitatu ijayo.
"Tunafanya kazi kwa pamoja ili Wasyria wengi zaidi warejee nyumbani. Serikali ya Ujerumani inaunga mkono ujenzi upya wa Syria kwa kutoa utaalamu, ushauri na taasisi zake,” alisema Merz.
Ujerumani ina idadi kubwa zaidi ya Wasyria barani Ulaya — zaidi ya milioni moja — wengi wao wakiwa waliwasili wakati wa wimbi la wakimbizi kati ya mwaka 2015 na 2016.
Kwa upande wake, Sharaa alisema Syria inataka kuanzisha mfumo wa uhamiaji wa "mzunguko,” ambao utawawezesha Wasyria kuchangia katika ujenzi wa nchi yao bila kupoteza maisha waliyojenga Ujerumani, kwa wale watakaochagua kubaki.
"Hatutasahau kamwe jinsi mlivyowafungulia milango zaidi ya Wasyria milioni moja. Mliwapa watu wetu nafasi ya kuanza upya maisha yao,” alisema Sharaa, akiipongeza Ujerumani kwa ukarimu wake.
Alisisitiza kuwa Syria inataka kuacha nyuma kipindi kigumu na kurejea kwenye maendeleo, akitaja fursa za uwekezaji katika sekta za nishati, usafiri na utalii.
Merz pia alisema Ujerumani iko tayari kusaidia ujenzi upya wa Syria, huku ujumbe wa serikali ukitarajiwa kutembelea nchi hiyo hivi karibuni. Hata hivyo, alisisitiza kuwa ushirikiano wa baadaye utategemea kuwepo kwa utawala unaoheshimu sheria.
Ziara yazua mjadala na ukosoaji
Pamoja na juhudi hizo za ushirikiano, ziara ya Sharaa imezua mjadala mkali nchini Ujerumani.
Wanaharakati wa haki za binadamu wamemkosoa, wakitaja historia yake ya kuhusishwa na makundi ya kiislamu yenye msimamo mkali na kuendelea kwa vurugu nchini Syria.
Maandamano yalifanyika mjini Berlin, ambapo baadhi ya watu waliunga mkono ziara hiyo huku wengine wakipinga. Waandamanaji walipeperusha bendera za Wakurdi na mabango wakipinga uongozi wake.
Msemaji wa mambo ya nje wa chama cha Kijani, Luise Amtsberg, alisema Ujerumani haipaswi kuharakisha kuhalalisha serikali ya Sharaa, akionya kuwa hali halisi nchini Syria bado ni tete.
Aidha, makundi ya kiraia yameeleza wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu na kuongezeka kwa mwelekeo wa utawala wa mabavu nchini Syria tangu Sharaa aingie madarakani.
Tangu kuondolewa kwa aliyekuwa rais Bashar al-Assad mwishoni mwa 2024, Syria imeendelea kukabiliwa na changamoto za usalama, huku mvutano wa kidini na uwepo wa makundi yenye silaha ukiendelea.
Ziara ya Sharaa nchini Ujerumani inaashiria hatua mpya ya kidiplomasia na juhudi za kurejesha wakimbizi pamoja na kujenga upya Syria.
Hata hivyo, ukosoaji unaoendelea unaonyesha kuwa bado kuna mashaka makubwa kuhusu utulivu wa nchi hiyo na mwelekeo wa uongozi wake.