Saudi Arabia yaitahadharisha Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Saudi Arabia yaitahadharisha Marekani

Saudi Arabia imetahadharisha kwamba uhusiano kati yake na Marekani unaweza ukaingia dosari kutokana na jinsi Marekani inavyoendesha sera zake katika kushughulikia mzozo wa Syria na mpango wa nyuklia wa Iran.

Mfalme Abdullah akiwa na Rais Obama

Mfalme Abdullah akiwa na Rais Obama

Taarifa hiyo imetolewa na mkuu wa ujasusi wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Bandar bin Sultan, ambaye ameahidi kuwa nchi yake itabadilisha mtazamo wake na kufanya mageuzi makubwa katika uhusiano na Marekani ikiwa ni katika kupinga jinsi Marekani inavyoshughulikia vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria na Iran.

Duru za karibu na sera za Saudi Arabia, zimeeleza kuwa Bandar amewaambia wanadiplomasia wa Ulaya kwamba Marekani imeshindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya Rais Bashar al-Assad wa Syria na mpango wa nyuklia wa Iran.

Marekani yashindwa kuiunga mkono Saudi Arabia

Amesema Marekani pia ilishindwa kuiunga mkono Saudi Arabia ilipokuwa upande wa Bahrain wakati ilipopambana na raia wanaoipinga serikali katika vuguvugu la mwaka 2011.

Amesema mageuzi hayo kwa Marekani yatakuwa makubwa na kwamba Saudi Arabia haitaki kujikuta katika hali ya kuwa tegemezi.

Mwanamfalme Turki Al Faisal

Mwanamfalme Turki Al Faisal

Hata hivyo, haikufahamika wazi iwapo matamshi hayo ya Mwanamfalme Bandar, aliyekuwa balozi wa Saudi Arabia nchini Marekani kwa miaka 22, yanaungwa mkono na Mfalme Abdullah.

Mvutano huo kati ya nchi hizo mbili pia umegonga vichwa vya habari vya Marekani, ambako mwanamfalme mwingine mwandamizi wa Saudi Arabia, amekosoa sera za Rais Barack Obama za Mashariki ya Kati, akimtuhumu kwa kukwamisha amani ya Syria na Israel na Palestina.

Mwanamfalme Turki al-Faisal, amesema sera za Obama kuhusu Syria zinasikitisha na ameukejeli mpango wa Urusi wa kutokomeza silaha za sumu za Assad.

Dalili zilianza mapema

Saudi Arabia ilianza kuonyesha dalili za kutoridhishwa na sera za Obama wiki iliyopita, baada ya kukataa kuchukua wadhifa wa kuwa mwanachama mpya asiyekuwa na kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika kile ilichoeleza ni kukasirishwa baada ya jumuiya ya kimataifa kushindwa kumaliza vita vya Syria na kushughulikia masuala mengine ya Mashariki ya Kati.

John Kerry na Saud al-Faisal

John Kerry na Saud al-Faisal

Katika mkutano wa jana Jumanne wa marafiki wa Syria uliofanyika London, Uingereza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry amesema atayazungumzia matamshi hayo ya Saudi Arabia atakapokutana na waziri mwenzake wa Saudi Arabia, Saud al-Faisal mjini Paris, Ufaransa Jumatatu ijayo.

Marekani na Saudi Arabia zimekuwa washirika tangu taifa hilo la Kifalme lilipotangazwa mwaka 1932, huku Saudi Arabia ikipewa usimamizi wa nguvu za kijeshi na Marekani ikihakikishiwaa usambazaji wa mafuta. Ukosoaji huo wa Saudi Arabia umetokea siku chache baada ya kuadhimisha miaka 40 ya vikwazo vya mafuta vya nchi za kiarabu Oktoba mwaka 1973, vilivyowekwa kuziadhibu nchi za Magharibi kwa kuiunga mkono Israel katika vita vya Yom Kippur.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com