1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rubio aelekea Qatar ´kutuliza joto´ msuguano na Israel

16 Septemba 2025

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Marco Rubio anaelekea nchini Qatar akitokea Israel leo Jumanne.

https://p.dw.com/p/50WHt
Israel | Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Marco Rubio
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Marco Rubio.Picha: Nathan Howard/AFP/Getty Images

Ziara hiyo inanuwia kupunguza mvutano baada ya Israel kuushambulia mkutano wa viongozi wa kundi la Hamas uliokuwa ukifanyika kwenye mji mkuu wa taifa hilo la Ghuba Jumanne iliyopita.

Ofisi ya Rubio imesema mwanadiplomasia huyo atakutana na viongozi wa Qatar na "kuwahakikishia uungaji mkono wa Marekani na kutoa ahadi kwamba shambulizi kama hilo halitotokea tena."

Viongozi mjini Doha wameghadhibishwa na shambulizi hilo na tangu lilipotokea wamekuwa wakitoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuiwajibisha Israel kwa kile wamekitaja kuwa "kitendo cha kichokozi".

Qatar ambayo kama ilivyo Israel ni mshirika wa karibu wa Marekani, imekuwa mstari wa mbele katika kutafuta suluhu ya vita vya Gaza hasa kupitia ukaribu wake na kundi la Hamas ambalo lina ofisi makao yake mjini Doha.